Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

CHMT BUKOBA WAPONGEZWA KWA UWAJIBIKAJI

Posted on: November 10th, 2024

Na. WAF-Bukoba

Madaktari Bingwa wa Rais Samia wameupongeza uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Bukoba na Timu ya Usimamizi wa Huduma za afya (CHMT) kutokana na huduma nzuri wanazozitoa kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa na Daktari Bingwa wa Kinywa na Meno, kutoka hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida, Dkt. Shila Mwashiuya wakati akizungumza kuhusu kambi ya madakatari bingwa wa Rais Samia walioweka kambi ya siku saba wilayani Bukoba mkoani Kagera kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa na bingwa bobezi kwa wananchi wa ngazi ya msingi.

“Tumekuja hapa hospitali ya Wilaya ya Bukoba tumekuta uongozi wa hospitali kwa kushirikiana na CHMT wanashirikiana vizuri kuhakiksha wanatoa huduma bora za afya kwa wananchi, kwani Serikali imewekeza vifaa tiba vya kisasa ili kufungamanisha huduma na wananchi wa ngazi ya msingi,” amesema Dkt. Mwashiuya

Aidha amewapongeza kwa kuwa wabunifu katika kuhudumia wananchi kwani kwa kutumia mapato ya ndani wamenunua mashine ya kisasa ya kutoa huduma za mkoba za kinywa na meno nje ya kituo ambapo mashine hiyo itasaidia kuwafuata wananchi katika maeneo yao.

“Mashine niliyoikuta hapa ni nzuri sana na nimewaelekeza wataalamu niliowakuta hapa namna ya kuitumia kutoa huduma za mkoba nje ya kituo, hivyo tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkumbwa katika sekta ya afya, mashine hii si gharama ndogo, lakini kama hospitali wameweza kununua na kwenda kutoa huduma katika jamii,”ameeleza Dkt. Mwashiuya

Hata hivyo, ametoa wito kwa Wataalamu wa hospitali hiyo kuweka ratiba ya kwenda kutoa huduma za mkoba za kinywa na meno katika jamii ili kuwasaidia wananchi wenye matatizo ya kinywa na meno.

Amesema kwa uwekezaji huo uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita ni jukumu la wataalamu wa afya kuchapa kazi, kwakuwa vifaa tiba vya kisasa vya kutolea huduma vimesimikwa katika maeneo yao ili kuboresha huduma za afya katika jamii

Kwa upande wake Mganga Mawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Bukoba, Dkt.
Jovin Stanislaus amesema kuwa kwa uwekezaji uliofanyika ni jukumu lao kuhakikisha wanawahudumia wananchi ili kuleta tija ya uwekezaji uliofanywa na Serikali.