BILIONI SITA KUKAMILISHA UJENZI WA HOSPITALI YA MANISPAA MOSHI, BILIONI 44 VIFAA TIBA
Posted on: October 6th, 2024Na WAF - Moshi, Kilimanjaro
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha zaidi ya Bilioni 44 kwa ajili ya ununuzi wa Vifaa Tiba pamoja na Bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Manispaa Moshi ambapo Hospitali hiyo ikikamilika itakua imegharimu Shilingi Bilioni Sita.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Oktoba 6, 2024 baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Manispaa ya Moshi pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Kata ya Mabogini ikiwa ni siku ya Tatu ya ziara yake katika Mkoa wa Kilimanjaro.
"Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kujali Watanzania, na sasa ametoa shilingi Bilioni 44 kwa ajili ya ununuzi wa Vifaa Tiba vitakavyotumika katika Hospitali ya Manispaa Moshi ikikamilika, lakini pia ametoa Bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali hii unaoendelea na ikikamilika itatumia Bilioni Sita." Amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama ameonesha utofauti wa fedha zilizotolewa katika kipindi kilichopita na kipindi cha sasa ambapo kwa kipindi hiki fedha zimetolewa nyingi zaidi lengo likiwa ni kuboresha miundombinu ya utolewaji wa huduma za Afya nchini.
"Katika Mkoa wa Kilimanjro kwa kipindi kilichopita ulipokea Bilioni Nane kwaajili ya Vifaa Tiba lakini kwa kipindi hiki kifupi chini ua uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Shilingi Bilioni 44 kwa ajili ya ununuzi wa Vifaa Tiba ikiwemo X-Ray, Ct-Scan, vitanda vya wagonjwa, vitanda vya kujifungulia pamoja na dawa." Amesema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama akiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Kata ya Mabogini amewaeleza wananchi kuwa Serikali imeleta fedha kwaajili ya miradi mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya ambapo fedha zilizoletwa ni kiasi cha shilingi Bilion 129 zitakazoshughulikia Sekta ya Afya katika Halmashauri hiyo.
Amesema, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Kata ya Mabogini ikikamilika itakua na wodi za kulaza wagonjwa pamoja na nyumba za watumishi ili wananchi wasipate tabu pindi wanapataka kupata huduma za afya hata ikiwa ni usiku.