Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

BILIONI 4.4 ZATOLEWA NA SERIKALI KUBORESHA HUDUMA ZA RADIOLOJIA NA UZALISHAJI WA HEWA YA OKSIJENI HOSPITALI RUFAA YA JESHI LUGALO

Posted on: June 25th, 2022


Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa kiasi cha Bilioni 4.4 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kutolea Huduma za Radiolojia, jengo la kufua hewa ya oksijeni pamoja na uboreshaji wa huduma za dharura na wagonjwa mahututi katika Hospitali Rufaa ya Jeshi Lugalo.


Prof. Abel Makubi Katibu Mkuu Wizara ya Afya.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi mara baada ya kutembelea miradi hiyo ya ujenzi inayoendelea kutekelezwa ndani ya Hospitali hiyo iliyopo Jijini Dar Es Salaam.
“Shilingi Bilioni 4.4 zimetolewa na Serikali chini ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya miradi ya ujenzi hapa Lugalo, lakini pia tumetoa zaidi ya Bilioni 4.8 kwa utekelezaji wa miradi ya afya kwenye Idara nyingine za Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza.” amesema Prof. Makubi na kuongezea kuwa Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Wizara na Taasisi nyinginezo kuboresha huduma za Afya.

Prof. Makubi ameipongeza Hospitali hiyo kwa usisamizi hodari wa miradi hiyo huku akiwataka viongozi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika ndani ya wakati ili wananchi waanze kupata huduma.

“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kutoa huduma za afya kwa wananchi lakini pia kwa kutoa fedha za UVIKO-19 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini” amesema Prof. Makubi ambaye pia alifikisha salaam za Waziri wa afya , Mhe Ummy Mwalimu kwa Uongozi wa Hospitali ya Lugalo.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Mnyepe amesema kuwa Wizara yake itaendela kushirikiana na Wizara ya Afya kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora za matibabu kwa wananchi.

Ujenzi wa jengo la Huduma za Radiolojia.

"Tunajenga hivi kwa ajili ya nchi wala sio kwa ajili ya jeshi pekee, huduma hizi tunazifanya kwa manufaa ya nchi” amesema Dkt. MnyepeKwa upande wake Mkuu wa Hospitali ya Jeshi Lugalo Brig. Jenerali Agatha Katua amesema kuwa Hospitali ya Jeshi Lugalo ilipokea fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 4.4 ambapo mpaka sasa tayari wameshanunua mashine ya kufua hewa ya oksijeni kutoka Borahi Kuu ya Dawa, huku ujenzi wa jengo la kuwekea mashine hizo na kutoa huduma ukiwa unaendelea.

Ujenzi wa jengo la kufua hewa ya oksijeni.

Brigedia Jenerali Agatha Katua amesema kuwa wanaendelea na ujenzi wa jengo la Radiolojia ambapo wataweka huduma zote za radiolojia sehemu hiyo kwa kuweka mashine za CT, Scan, MRI, X-Ray, Ultra Sound.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa jengo la radiolojia na jengo la kufua hewa ya oksijeni, Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT Kanali Petro Ngata amesema ujenzi wa jengo la radiolojia umefikia asilima 62 huku wakitarajia kukamilisha ujenzi ifikapo Mwezi Septemba 2022 huku Jengo la kufua hewa ya oksijeni ujenzi umefikia asilimia 45 na wanatarajia kukamilisha ifikapo Mwezi Agosti 2022.

Mwisho