3,077 WAJITOKEZA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA KAGERA KUPATA HUDUMA ZA KIBINGWA
Posted on: May 9th, 2025
Na WAF, Kagera
Wananchi wapatao 3,077 wamejitokeza mkoani Kagera na kumenufaika na matibabu ya Kibingwa yaliyotolewa na Madaktari Bingwa wa Rais Dkt. Samia iliyofikia tamati leo Mei 09, 2025 mkoani humo.
Akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera Dkt. Museleta Nyakiloto amesema mwitikio wa wagonjwa umezidi lengo walilojiwekea, hivyo zoezi hilo limetekelezwa kwa mafanikio makubwa.
Dkt. Nyakiloto amesema matangazo mengi yaliyotolewa na kamati ya maandalizi ya kambi hiyo yamechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko hilo la wagonjwa na kutoa shukurani zake kwa kamati hiyo.
Naye Daktari Bingwa wa Masuala ya Mkojo Dkt. Flavian Simulamu amesema yeye binafsi amehudumia wagonjwa 158 na kati yao wamefanya upasuaji kwa watu 11 wakiwemo wazee na watoto.
Dkt. Simulamu amesema amefanya upasuaji kwa watoto sita (6) wenye matatizo ya kuzaliwa nayo ikiwemo mtoto aliyezaliwa na maumbile ya kiume yaliyogeukia chini na kusema kuwa upasuaji huo ni wa kwanza na wa aina yake katika hospitali hiyo.
Dkt. Simulamu ameongeza kuwa wamewapa wagonjwa wengine rufaa za kwenda Bugando kwa uchunguzi zaidi na upasuaji wa Kisasa usiohitaji kufunguliwa ngozi kwa kuwa huduma hiyo inafanyika Bugando peke yake katika kanda ya ziwa.
Kwa upande wa Kliniki ya mifupa Dkt. Bingwa wa magonjwa ya mifupa Dkt. Zabron Charles Saguda amesema imepokea wagonjwa takribani 400 wakiwemo wagonjwa wa upasuaji na wagonjwa wa nje.
Kambi ya Madaktari Bingwa mkoani Kagera ilianza tarehe 05.05.202 na imefanyika kwa mafanikio makubwa na baadhi ya wananchi wamependekeza kama ikiwezekana siku ziongezwe ili watu wengi zaidi wapate huduma hiyo.