Ministry of Health

WIZARA YA AFYA YAFIKIA ASILIMIA 72 YA MAKUSANYO, FEDHA ZA NJE ZAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: May 11th, 2026

Wizara ya Afya pamoja na taasisi zake imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini kupitia ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha katika utekelezaji wa miradi na huduma mbalimbali za afya kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Mei 11, 2026, wakati akiwasilisha Bajeti ya mwaka Mpya wa Fedha 2026/27 mbele ya Bunge la Bajeti la 13, Mkutano wa Tatu, kikao cha 26, Bungeni jijini Dodoma

Mhe. Mchengerwa amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara na taasisi zake zilikadiria kukusanya Shilingi bilioni 819.98 ambapo hadi kufikia Machi 2026 zilikuwa zimekusanya Shilingi bilioni 593.85, sawa na asilimia 72.42 ya lengo lililowekwa.

“katika mwaka huo wa fedha, Wizara iliidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 1.76 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Hadi Machi 2026, Wizara ilikuwa imepokea Shilingi trilioni 1.11 sawa na asilimia 63 ya fedha zilizoidhinishwa. Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida yalipokea asilimia 76 huku miradi ya maendeleo ikipokea asilimia 56,” amesema Mhe. Mchengerwa

Aidha Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa Wizara imeendelea kuimarisha sekta ya afya, fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo ziliendelea kuwa msaada mkubwa katika utekelezaji wa huduma muhimu za afya nchini. Wadau hao ni pamoja na Global Fund, GAVI, Benki ya Dunia, HBF, UNICEF, UNFPA pamoja na wengine waliochangia katika mapambano dhidi ya UKIMWI, kifua kikuu, malaria, huduma za chanjo, lishe, damu salama pamoja na afya ya mama na mtoto.

Amesisitiza Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa, Sera ya Afya ya mwaka 2007, Ilani ya CCM ya mwaka 2025, Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Afya Awamu ya Tano (HSSP V), Mpango Mkakati wa Muda wa Kati pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 (SDGs).