Ministry of Health

WIZARA YA AFYA KUIMARISHA MIKAKATI MADHUBUTI KUDHIBITI MAGONJWA YA MILIPUKO MIPAKANI

Posted on: May 10th, 2026

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) imeendelea kuimarisha mikakati ya kudhibiti magonjwa ya milipuko katika maeneo ya mipakani kwa kuhakikisha viashiria vyote vinavyoweza kuhatarisha afya ya jamii vinadhibitiwa kwa ufanisi, hatua hiyo inalenga kulinda usalama wa Wananchi katika mipaka ya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na kuzuia kuenea kwa magonjwa hatari ikiwemo kipindupindu.

Hayo yamesemwa leo Mei 10, 2026 Mkoani Morogoro na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Afya Mazingira na Usafi, Dkt. Amour Seleman amesema, wataalamu wa afya wanaendelea kuandaa mipango ya kudhibiti viashiria vya uchafuzi wa mazingira vinavyoweza kuathiri afya ya jamii katika maeneo ya mipakani. Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mipango hiyo utasaidia kuhakikisha jamii zinabaki salama dhidi ya magonjwa ya milipuko.

Aidha, Dkt. Seleman amewataka Viongozi na Washiriki wote wa kikao kazi hicho kuhakikisha wanatekeleza kwa umakini mipango yote iliyowekwa ili kuimarisha ulinzi wa afya kwa wananchi wanaoishi na kusafiri kupitia maeneo ya mipakani.

Naye Mkuu wa Huduma za Afya Mipakani, Dkt. Remedius Kakulu amesema kikao kazi hicho kinalenga kuimarisha usimamizi wa afya katika maeneo yote ya mipakani nchini na wataalamu wanaendelea kuandaa miongozo ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira pamoja na mipango ya utekelezaji katika vituo vyote 59 vya mipakani Tanzania Bara na vituo vya Zanzibar.

Dkt. Kakulu amesema mipango hiyo inahusisha udhibiti wa magonjwa ya milipuko, usalama wa maji safi, udhibiti wa taka ngumu na majitaka, usalama wa chakula na vinywaji, udhibiti wa wadudu wanaosababisha magonjwa pamoja na ufuatiliaji wa ubora wa hewa katika maeneo ya mipakani.

Kwa upande wake Mkuu wa Huduma za Afya Mipakani Zanzibar, Bi. Rukaiya Mohamed Said amesema Zanzibar imepata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya mipango hiyo kupitia maeneo yake ya mipakani ikiwemo bandari tisa. Ameeleza kuwa mipango hiyo Pia inajumuisha usimamizi wa usalama wa maji, vyakula na vinywaji pamoja na udhibiti wa wadudu na ufuatiliaji wa hewa safi.