Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WIZARA YA AFYA KUFANYA TATHMINI BAADA YA KUKABILIANA NA UVIKO-19

Posted on: September 18th, 2023

Na. WAF - Dar es Salaam 


Baada ya miaka Minne ya kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19, Wizara ya Afya imechukua jukumu la kufanya zoezi la tathmini kwa namna ilivyokabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo nchini.


Hayo yamesemwa leo na Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Msasi wakati akifungua kikao cha Kwanza kwa zoezi hilo la tathmini kwa niaba ya katibu Mkuu Wizara ya Afya.


“Wizara imeona ni wakati sahihi kufanya tathmini hiyo na kwa mujibu wa kanuni za udhibiti wa magonjwa ya mlipuko ni vizuri kufanya tathmini ili kuimarisha namna ya kukabiliana na magonjwa kama hayo kwa nyakati za usoni”. Amesema Bw. Msasi 


Amesema, lengo ni kuainisha masuala yaliyofanyika vizuri, kubaini changamoto na mapungufu katika mapambano ya UVIKO-19, na namna ya kuweza kukabiliana na matukio kama hayo endapo yatajitokeza kwa nyakati zijazo.


Aidha, Bw. Msasi amewataka washiriki wote kwenye kikao hicho cha tathmini kuwa huru katika kutoa taarifa sahihi na maoni yao kwa kuwa kikao hicho hakina lengo la kumlaumu yeyote wala kunyosheana vidole bali kimelenga zaidi kufanya tathmini na kuboresha njia nzuri zaidi za kuweza kukabiliana na majanga kama ya UVIKO-19 endapo yatajitokeza tena nchini. 


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa Wizara ya Afya Dkt. Angela Samwel amesema tathmini hiyo baada ya kukabiliana na mlipuko wa UVIKO-19 imehusisha wadau mbalimbali kutoka Wizara, Taasisi za Serikali, Waganga Wakuu wa Mikoa, Hospital za Serikali na Binafsi na wengine kutoka Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wa maendeleo.


Dkt. Angela amesema taarifa ya tathimini hiyo itahusisha masuala mazuri yaliyofanyika wakati wa kukabiliana na UVIKO-19, Changamoto na Mapungufu pia itapendekeza hatua za muda mfupi na muda mrefu za kuchukua ili kuendeleza masuala mazuri na kuboresha mapungufu yaliyojitokeza na itawasilishwa kwa viongozi na wadau mbalimbali.


Ugonjwa wa UVIKO- 19 umeendelea kutolewa taarifa duniani kote, hata hivyo katika siku za hivi karibuni ugonjwa huo umeendelea kupungua na kupelekea kuondolewa masharti mbalimbali yaliyowekwa kukabiliana nao, hii ni pamoja na tamko la WHO kuwa ugonjwa huo sio dharura ya Kiafya ya Kimataifa.