Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAZIRI MHAGAMA AGAWA MASHINE 185 ZA UCHUNGUZI WA KIFUA KIKUU NCHI NZIMA

Posted on: January 7th, 2025

Katika jitihada za kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini Tanzania ifikapo 2030, Serikali imegawa mashine mpya 185 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 7 kwa ajili ya uchunguzi na ugunduzi wa vimelea vya ugonjwa huo nchini.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Januari 6, 2025 kwenye hafla ya ugawaji wa mashine hizo iliyofanyika katika Kituo cha Afya Chamwino, Dodoma iliyoenda sambamba na uzinduzi wa Mpango harakishi wa kuibua wagonjwa wa Kifua Kikuu katika Halmashauri 76 za mikoa tisa (9).

Waziri Mhagama amesema Tanzania inafanya vizuri kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu ambapo kwa sasa ni nchi ya Sita kati ya nchi zote zinazofanya vizuri lakini bado juhudi zinaendelea ili kufanya vizuri zaidi kwa kuwa bado tupo ndani ya nchi 30 zenye maambukizi makubwa.

"Ugonjwa wa Kifua Kikuu bado ni ugonjwa tishio nchini na ulimwenguni kwa ujumla kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye maambukizi makubwa ya ugonjwa huo ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia 87 ya wagonjwa wote wa Kifua Kikuu Duniani," amesema Waziri Mhagama

"Leo tunazindua mashine za kisasa 75 aina ya GeneXpert zinazotumika katika ngazi ya Hospitali, na mashine 110 aina ya Truenat ambazo zimetengenezwa kuwezesha kufanya kazi hadi katika ngazi ya Zahanati ambazo zinegharimu shilingi Bilioni 7 na zitasambazwa katika mikoa yote na mikoa miwili (2) upande wa Zanzibar,” amefafanua Waziri Mhagama

Katika hatua nyingine Waziri Jenista amezindua Mpango harakishi wa kuibua wagonjwa wa Kifua Kikuu kwenye Halmashauri 76 kutoka Mikoa 9 amabyo kwa 2024 imeonyesha kuwa na kiwango kidogo cha uibuaji wa wagonjwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambao ni mkoa wa Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Kagera, Mara, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu na Tanga

Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Ahmad Makuwani amesema kuwa juhudi kubwa sasa zinaelekezwa katika uibuaji wa wagonjwa wapya wa Kifua Kikuu, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika teknolojia ya matibabu hasa kwenye vifaatiba, hivyo sasa tuna jukumu la kutoacha mtu nyuma kwenye mapambano hayo na kutokomeza Kifua Kikuu ifikapo mwaka 2030.