Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATOTO WATATU KATI YA 10 CHINI YA MIAKA MITANO WANA UDUMAVU TANZANIA

Posted on: June 15th, 2024


Na WAF - Dar Es Salaam


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kwa sasa takwimu zinaonyesha kuwa takribani watoto Watatu kati ya Kumi wenye umri chini ya miaka mitano hapa nchini wana udumavu kutokana na lishe duni.


Waziri Ummy amesema hayo leo Juni 15, 2024 jijini Dar Es Salaam wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza viturubishi (Premix Blending Plant) cha Kampuni ya SANKU - PHC Tanzania kilichozinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.


"Lakini pia watoto 59 kati ya 100 wenye umri huo wa chini ya miaka Mitano wana tatizo la upungufu wa damu na vile vile watoto 30 kati ya 100 wana ukosefu wa Vitamini A, pia kwa upande wa akina mama walio kwenye umri wa kuzaa, asilimia 20 yao wana tatizo la upungufu wa damu." Amesema Waziri Ummy


Waziri Ummy akiendelea kuelezea athari za ukosefu wa lishe bira amesema, watoto Watatu kati ya watoto 100 wanazaliwa na tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi hapa nchini Tanzania ikiwa ni nchi ya Tatu kwa kuwa na viwango vikubwa baada ya Algeria na Ethiopia.


Aidha, Waziri Ummy amesema kwa upande mwingine mchango wa lishe kwenye kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano, vimepungua kutoka vifo 147 mwaka 1999 hadi vifo 43 mwaka 2022 kwa kila vizazi hai1000, wakati kwa vifo vya watoto wachanga, vimepungua kutoka watoto 40 mwaka 1999 hadi watoto 24 mwaka 2022 kwa kila vizazi hai 1000.


"Hizi ni baadhi tu ya takwimu ambazo zinahusiana na upungufu wa virutubishi muhimu vya lishe katika vyakula vyetu, lakini mchango wa lishe endapo unazingatiwa na jamii yetu, madhara yake sote tunayajua katika uzazi, makuzi ya watoto kiakili na kimwili, maendeleo ya elimu na uchumi kwa ujumla." Amesema Waziri Ummy


Amesema, hatua ya kuanzishwa kwa kiwanda hichi ni muhimu kwa kuwa katika kipindi chote hiki virutubishi hivyo vilikuwa vinaagizwa kutoka nje ya nchi lakini leo hii hapa nchini tutakuwa na tovuti ambayo itawaunganisha wadau walioko kwenye mnyororo wa kuongeza virutubishi kwenye vyakula pamoja na kuvisambaza kwa walaji.