Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATANZANIA TUJENGE UTAMADUNI WA KUPIMA AFYA ZETU: MHE. UMMY MWALIMU

Posted on: August 21st, 2023

Na E. Kayombo – WAF Tanga

Wito umetolewa kwa watanzania kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kutambua hali zao kiafya mapema na kuepukana na maradhi ambayo yanaweza kugharimu fedha nyingi za matibabu na hata kusababisha ulemavu hadi vifo.

Wito huo umetolewa leo na Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya nchini Tanzania alipokuwa akifungua kambi ya upimaji afya ya Afya check iliyoandaliwa na Uongozi wa Afya Cheki Dr. Isac Maro kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tanga na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

“Watanzania wengi tunakwenda Hospitali tayari ugonjwa umeshakuwa mkubwa sana, wagonjwa wa Saratani wanakwenda Hospitali, Saratani ikiwa hatua ya nne, hatuna mazoea ya kupima afya mapema kujua hali zetu” ameeleza Mhe. Ummy mwalimu kwa kutolea mfano wa hali ya ugonjwa wa Saratani.

Amesema kuwa maradhi yakigundulika mapema huwa ni rahisi kuyatibu lakini pia kupunguza madhara, hivyo kupitia kambi hiyo ya Afya Cheki anawahimiza, kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi wa Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla umuhimu wa kupima afya. katika Taasisi ya Saratani ya Ocean ameshuhudia akiona wagonjwa wanafika wakiwa wanaugua Saratani ya tezi dume, Saratani ya Mlango wa Kizazi, ugonjwa umeshasambaa mwili mzima.

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya upatikanaji wa huduma za afya nchini. “Huduma za matibabu ni gharama, wananchi wengi bado hawamudu gharama za matibabu, suluhisho pekee ni kujiunga na bima ya afya ili tuwe na uhakika wa matibabu pale tutakapokuwa tumeugua” aemesema Mhe. Ummy Mwalimu.