Ministry of Health

WATAALAMU WA MAABARA WAJENGEWA UWEZO KUIMARISHA HUDUMA ZA UCHUNGUZI , UTAYARI WA KUKABILIANA NA MILIPUKO

Posted on: June 24th, 2026

Na WAF, IRINGA

Wananchi wa Mkoa wa Iringa wanatarajiwa kupata huduma bora zaidi za maabara na uchunguzi wa magonjwa kufuatia juhudi za Serikali za kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa maabara ili kuongeza usahihi wa vipimo, usalama wa huduma na utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Hayo yameelezwa Juni 24, 2026 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Sylvia Mamkwe, wakati akifungua mafunzo ya Siku tano kwa wataalamu wa Maabara wa ufuatiliaji magonjwa kutoka mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Ruvuma yanayofanyika katika Chuo cha Afya cha Primary Health Care Institute (PHCI) kilichopo Manispaa ya Iringa.

Dkt. Mamkwe amesema mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa wataalamu wa Maabara katika uchukuaji, uhifadhi na usafirishaji salama wa sampuli kutoka kwa wahisiwa (suspect) wa magonjwa ya mlipuko kama Ebola na Marburg, hatua itakayosaidia kuimarisha ubora wa huduma za uchunguzi na usalama wa wahudumu wa afya, wananchi na mazingira kwa ujumla.

Ameongeza kuwa, maabara ni nguzo muhimu katika mifumo ya afya kwani husaidia kubaini magonjwa kwa wakati, kuwezesha utoaji wa tiba sahihi na kusaidia Serikali kufanya maamuzi ya haraka na kwa wakati kwenye kukabiliana na milipuko ya magonjwa pamoja na umuhimu wa ufuatiliaji wa magonjwa katika huduma za maabara (Laboratory based Surveillance).

Katika mafunzo hayo, washiriki wamepata elimu kuhusu dalili za magonjwa ya mlipuko, tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa wakati wa uchukuaji wa sampuli za wagonjwa wanaohisiwa kuwa na maambukizi pamoja na matumizi sahihi ya vifaa kinga binafsi (PPE).

Washiriki pia wamejengewa uwezo kuhusu taratibu za ufungashaji na usafirishaji salama wa sampuli kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa, hatua inayolenga kupunguza hatari za maambukizi na kuongeza ufanisi wa huduma za uchunguzi wa magonjwa.