Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATAALAM WA MAABARA ZA AFYA WAHIMIZWA KUTOA HUDUMA KWA KUFUATA TAALUMA, MAADILI

Posted on: June 16th, 2025

Wataalam wa Maabara za Afya wametakiwa kufuata sheria na taratibu zinazosimamia uendeshwaji wa Maabara hizo ili kutoa huduma bora kwa jamii.


Hayo yamesemwa leo t Juni 16, 2025 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bw.Kaspar Mmuya wakati wa  mkutano kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,wamiliki wa Maabara Binafsi za Afya pamoja na wataalam wa maabara uliofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma.


Amesema watu wa maabara ni wadau muhimu kwani wanafanya kazi kwa kushirikiana na madaktari ili kutambua magonjwa mbalimbali kwa kufanya vipimo na kutoa majibu sahihi kwa wagonjwa na sio vinginevyo.


“Lengo la maabara ni kuchunguza kitu kulingana na maelezo ya mgonjwa na sio kutafuta mapato, kwa mfano mtu anasema anaumwa mguu huku unampima UTI kwa sababu una maslahi labda ya dawa au maelekezo mengine ya kimapato hayo sio maadili ya kazi yako.” amesema Bw. Mmuya.


Amewataka pia wanataaluma kukaa kwenye taaluma yao na kuifanyia kazi na sio kuhama kwa makusudi na kuchukua taaluma nyingine ambayo hawajaisomea na kutoa  huduma kwa wagonjwa.


“Wagonjwa wakifika hospitalini hawajui nani ni nani wakiona tu umevaa koti jeupe wanajua ni daktari, sasa baadhi ya wanataaluma wa maabara wanauvaa uhusika wa udaktari wakati wanajua sio madaktari, hivyo nawasihi mfanye kazi kwa taaluma mliyosomea,” amesema Bw. Mmuya.


Aidha Bw. Mmuya ametoa rai kwa wamiliki wa maabara binafsi kuhakikisha maabara zinakuwa na vitu vyote muhimu kulingana na miongozo inavyohitaji.


“Majengo yawe na sifa za kutoa huduma husika, kulingana na miongozo, hii itasaidia kutoa huduma bora na mazingira mazuri lakini kinyume chake kutaleta shida kwa wagonjwa wakati wa kupata huduma," amesema Bw. Mmuya


Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Thomas Rutachunzibwa amewaasa watendaji wa maabara kuhakikisha wanatoa majibu sahihi na kufuata miiko ya kazi kwani taaluma hiyo inahitaji uwajibikaji lakini kwa sekta binafsi wanahitaji na fedha pia.


“Wagonjwa wanatufanyia tathmini bila ya sisi kujua, wanapima maabara hii wakitoka wanakwenda maabara nyingine, hii ni kupima na kuona wapi wana pata majibu sahihi. Kuna mwaka lilipita wimbi la UTI kila mgonjwa ana UTI, sasa tuangalie utandaji kazi wetu na kutoa majibu sahihi na sio kubambikizia majibu tu ili upate fedha,” amesema Dkt. Rutachunzibwa.


Awali Msajili wa Maabara Binafsi za Afya Bw. Dominic Fwiling'afu, aliwataka wamiliki wa maabara binafsi na wanataaluma wa maabara, kuonana uongozi mara moja ili kutatua changamoto zao kwa haraka pindi wanapopata shida, wasikumbatie matatizo mpaka mambo yanapokuwa makubwa, huku akitilia mkazo kwa wamiliki kujua miongozo na sheria zinazowasimamia.