WANANCHI NJOMBE WAHAMASISHA WENZAO KUPATA HUDUMA ZA MADAKTARI WA RAIS SAMIA
Posted on: May 27th, 2025
Na WAF, Njombe
Wananchi mkoani Njombe wameshimdwa kuficha hisia zao mara baada yakupatiwa matibabu na kuamua kuhamasishana wao kwa wao kuhudhuria kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia inayoendea hivi sasa katika halmashauri zote za mkoa huo, kwani muda wa siku sita bado haujakamilika.
Akizungumza mara baada ya kupatiwa huduma Mei 27, 2025 katika Hospitali ya Halmashauri ya Njombe mji Kibena Bw. Sufian Kihongosi (65) mkazi wa eneo hilo amesema wanashukuru uwepo wa madaktari hao, kwani wameweza kupatiwa huduma nzuri bila kulazimika kusafiri kusaka huduma hizo za kibingwa.
“Nishukuru madaktari bingwa wamekuja eneo hili imekuwa jambo jema na nzuri, tunashukuru pia Serikali kwa kutuletea huduma karibu na maeneo yetu, ameeleza. Bw. Kihongosi
Amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Hassan kwa kwa kupata huduma za matibabu za kibingwa kwa urahisi kwani wanatumia.kiasi kidogo cha fedha kufika eneo la.kupatia huduma.
Kuhusu wananchi ambao hawajafika Bw. Kihongosi amesema ni vizuri wafike ndani ya siku sita zilizotengwa ili wachunguzwe afya na wakikutwa na changamoto ya afya watibiwe.
Kwa upande wake Bw. Albert Mahundi (59) ametoa wito kwa Serikali kuwa huduma hiyo ya Madaktari bingwa wa Rais Samia kushuka katika ngazi ya msingi kutoa huduma na na kuwa endelevu ili kuhakikisha wananchi wa ngazi ya msingi wanapata huduma kwa karibu na ubora unaoendana na uwekezaji uliofanywa na Serikali.
" Sio Serikali imewekeza miundombinu bora, vifaa tiba vya kisasa halafu wataalam hawapo ila kwa kambi hii itasaidia kufufua vifaa ambavyo vipo na vilikuwa havitumiki," amesema Bw. Mahundi.
Aidha ameushukuru uongozi wa Halmashauri ya mji wa Njombe wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa kutoa matangazo ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa na bingwa bobezi
Kwa upande wake Mwanafunzi wa Utabibu Antony Donge kutoka Chuo cha Afya Mgao kilichopo mkoani humo amesema uwepo wa madaktari hao umewasaidia kujifunza vitu mbalimbali ambavyo vitawasaidia katika utendaji kazi wao kwani wapo katika mafunzo kwa vitendo kwa sasa.
“Tumefurahia kwa sababu tunapata uzoefu mkubwa na wanatuelekeza vitu ambavyo tulikuwa hatuvijui, hakika hii ni furaha kubwa mno kwetu,” ameeleza Bw. Donge
Amesema kupitia wataalam hao wanaamini watakuwa wataalam wazuri ambao watalisaidia Taifa kwa siku za mbeleni.
Madakatari waliopo mkoani Njombe wanatibu magonjwa ya ndani, wanawake,Watoto wachanga, upasuaji na pua, koo na masikio na wanaendelea kutoa huduma za kibingwa na bobezi katika halmashauri sita za mkoa wa Njombe tangu Mei 26 na watamaliza zoezi hilo Mei 31 2025.