Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAKURUGENZI KUNUNUA VIATILIFU VYA KUULIA MAZALIA YA MBU

Posted on: November 14th, 2023


Na WAF, Tabora
Wakurugenzi wa Halmashauri ya mkoa wa Tabora wametakiwa kununua viatilifu vya kuua mazalia ya mbu na viluilui kwa mapato yao ya ndani ili kupunguza idadi ya maambukizi ya ugonjwa wa Malaria.

Hayo yamesemwa na Balozi Dkt. Batilda Buriani wakati akiwapokea Wabunge wanaounda Mtandao wa Wabunge wanaopambana na Malaria na Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele (TAPAMA) wakifanya ziara kuangalia hali ya huduma na maendeleo ya mapambano dhidi magonjwa hayo katika Mkoa wa Tabora.

Dkt. Batilda amebainisha hatua za kukabiliana na ugonjwa wa malaria ikiwa ni Pamoja na kuwataka wakurugenzi kununua viatilifu vya kuua mazalia ya mbu na viluilui Pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutumia chandarua na kua na utaratibu wa kwenda kutibiwa hospitali.

Aidha Dkt. Batilda ameelezea kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria katika mkoa wa Tabora kilikua ni 11.7% kwa Watoto kati ya umri wa miezi 6 hadi 59 kwa mwaka 2017/2018 hivyo kuongezeka hadi 23.4% hivyo kufanya mkoa wa Tabora kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria katika Jamii.

“Jiografia ya mkoa wa Tabora kuwa na maeneno mengi yenye madimbwi ya maji yanayotuama katika maeneo mbalimbali ya makazi ya watu hasa kwenye kipindi cha mvua zimechangia kuwa na kiwango cha juu cha maambukizi ya Malaria”. Amesema Dkt. Batilda.

Pia, Dkt. Batilda amesema kuwa Imani potofu iliyojengeka katika jamii juu ya matumizi ya vyandarua vyenye dawa imeongeza hali ya maambukizi ya Malaria hali iliyopelekea baadhi ya wananchi kutotumia vyandarua wanavyogawiwa katika vituo vya kutolea huduma za afya hivyo kutoa wito kwa jamii kufika katika kituo cha huduma za afya kwa ajili ya matibabu badala ya waganga wa kienyeji.

Dkt. Batilda ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiongezea bajeti ya dawa Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa mbali mbali.