WAGONJWA ZAIDI YA 28,000 WANUFAIKA NA MISAMAHA YA BIL 5 MATIBABU MNH
Posted on: March 18th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Dar es Salaam
Wagonjwa zaidi ya 28,000 wamepatiwa misamaha ya huduma za matibabu zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.3 kwa mwaka wa fedha 2025/26 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Serikali ya kuwasaidia wagonjwa wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Hayo yameelezwa Machi 16, 2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi akimuwakilisha waziri wa afya Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kukagua utoaji wa huduma za afya pamoja na maendeleo ya miradi ya hospitali hiyo.
Dkt. Samizi amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya huku wale wasiokuwa na uwezo wakinufaika na misamaha ya matibabu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Johannes Lukumay ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa juhudi za kuimarisha huduma za afya pamoja na kusaidia wananchi wasiokuwa na uwezo kupata matibabu.
Aidha, ameitaka hospitali hiyo kuhakikisha majibu ya vipimo vya maabara yanatolewa kwa wakati ili kurahisisha matibabu kwa wagonjwa na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa mipango yote ya maboresho na huduma zinazotarajiwa kutekelezwa kujumuishwa kikamilifu katika mpango mkakati wa hospitali (Strategic Plan) ili kurahisisha utekelezaji na ufuatiliaji wa malengo ya taasisi.
Dkt. Lukumay pia ameishauri hospitali hiyo kutafuta utaratibu wa kuwabakisha wataalamu wanaopata mafunzo ya kitaalamu hospitalini hapo ili kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi, pamoja na kuweka mfumo wa kufuatilia wagonjwa hata wanapokuwa majumbani baada ya kupata matibabu ili kuboresha huduma endelevu kwa wagonjwa.