Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAGONJWA 13 WAGUNDULIKA NA UGONJWA USIOFAHAMIKA MKOANI LINDI

Posted on: July 13th, 2022

Na. WAF - Dodoma 

Wagonjwa 13 wamegundulika kuwa na ugonjwa usiofahamika katika kijiji cha Mbekenyera Halmashauri ya Ruangwa mkoani Lindi na watatu kati yao wamefariki.

Akitoa taarifa hiyo Mganga mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe leo Julai 13, 2022 mbele ya  waandishi wa habari mkoani Dodoma. Dkt. Sichalwe amesema Julai 7, 2022 Wizara ya Afya ilipokea taarifa toka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Amesema kuwa taarifa hiyo ilitaja  kuwa katika Halmashauri ya Ruangwa kumekuwepo na ugonjwa  usiofahamika kutoka kituo cha Afya Mbekenyera ambapo Ndani ya siku 3 (tarehe 5 na 7 Julai, 2022) walipokea wagonjwa 2 katika kituo hicho wakiwa na dalili za homa, kuvuja damu (hususani puani) kichwa kuuma na mwili kuchoka sana.

"Ili kufatilia taarifa hiyo Wizara iliunda timu ya wataalam kutoka idara ya Magonjwa ya dharura na Majanga, Epidemiolojia, Mkemia Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Utafiti (NIMR), Chuo kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili na Hospitali ya Taifa Muhimbili, waliungana na timu ya Mkoa ikihusisha pia Idara ya Mifungo." Amesema Dkt. Sichalwe 

Wizara ya Afya inaendelea kufanya uchunguzi zaidi wa kiepidemiolojia na kitabibu huku ikisubiri matokeo ya vipimo zaidi vya maabara ya magonjwa ya Binadamu na Wanyama kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Aidha, wizara inaendelea kutafuta watu wengine wenye dalili kama hizi ili kutambua mapema na kuwatenga kwa kuzuia ugonjwa usisambae zaidi, pia Kuwatambua watu wote waliotangamana (Contacts) na wagonjwa, wahisiwa, pamoja na marehemu wa ugonjwa huo.

Pia, Kutoa matibabu kwa wagonjwa waliobainika kuwa na dalili, kuwashauri wajitenge wakati wakisubiria majibu ya vipimo vya maabara, Kutoa elimu kwa jamii kwa kutumia vyombo mabalimbali vya habari.

Hata hivyo, wizara ya Afya inaendelea kufanya Maandalizi ya dawa, vifaa tiba na vifaa vya kujikinga na maambukizi kwa ajili ya kuwahudumia waathirika endapo watajitokeza.

Pamoja na hayo, Wizara imetoa wito kwa wananchi kuwa watulivu wakati ikiendelea kulifanyika kazi suala hili pia Wananchi waendelee kutumia Vituo vya kutolea huduma za afya pale wanapojisikia kuumwa.


Mwisho