Ministry of Health

USHIRIKIANO WA KIKANDA WAENDELEA KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA SEKTA YA AFYA

Posted on: May 17th, 2026

Geneva – Uswisi

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, leo Mei 17, 2026 ameshiriki katika shughuli mbili muhimu zilizofanyika kabla ya kuanza rasmi kwa Mkutano Mkuu wa 79 wa Shirika la Afya Duniani (WHA79) unaotarajiwa kuanza Mei 18, 2026 mjini Geneva, Uswisi.

Dkt. Magembe alishiriki katika programu ya Walk the Talk inayohamasisha jamii kuzingatia afya, kufanya mazoezi na kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa.

Aidha, akimwakilisha Waziri wa Afya, alishiriki katika kikao cha pembeni cha Mawaziri wa ECSA-HC kilichofanyika Hoteli ya Crowne Plaza Geneva, ambapo viongozi na wadau wa afya walijadili mikakati ya kuimarisha mifumo ya afya, ushirikiano wa kikanda pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto za afya katika nchi wanachama.

Katika kikao hicho, Mawaziri walithibitisha uteuzi wa Dkt. Ntuli Kapologwe kuwa Mkurugenzi Mkuu wa ECSA-HC.

Akizungumza kuhusu ushiriki huo, Dkt. Magembe amesema majukwaa ya kimataifa yanaendelea kuwa muhimu katika kuimarisha ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kujenga mifumo imara ya afya kwa manufaa ya wananchi.