Ministry of Health

TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA VIPAUMBELE VYA AFYA KUWA CHACHU YA UBORA WA HUDUMA

Posted on: March 18th, 2026

Na Emmanuel Malegi, WAF- Dodoma

Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi na Matengenezo ya Vifaa Tiba, Dkt. Alex Magesa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya amesema kupitia Mkutano wa Tathmini ya Utekelezaji wa Vipaumbele vya Sekta ya Afya, utasaidia kuainisha changamoto za utekelezaji wake uliopita na kupanga mikakati ya kuboresha utekelezaji wa vipaumbele vya sekta ya afya kwa mwaka ujao wa fedha (2026/27).

Dkt. Magesa amesema hayo Machi 17, 2026 wakati wa kikao cha kupitia mkakati huo kinachoendelea jijini Dodoma.

Amesema licha ya mafanikio makubwa ya utekelezaji wa vipaumbele yanayotokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika Sekta ya Afya ikiwemo ununuzi vifaa na vifaa tiba na mashine kubwa za kisasa zinazotumika katika uchunguzi Bobezi ikiwemo CT SCAN, PET SCAN na MRI

"Kupitia uwekezaji wa mashine hizo kama nchi umesaidia kupunguza gharama kubwa kwa wananchi kufuata huduma za matibabu nje ya Tanzania, na kuokoa muda kwani zinatumia muda mfupi zaidi hivyo kuwapa wananchi nafasi ya kuendelea na shughuli zao za kiuchumi" amesema Magesa.

Dkt. Magesa ametoa wito kwa watanzania wote kuendelea kujiandikisha kwenye Bima ya Afya kwa Wote ili kuwa na tahadhari na uhakika wa matibabu pindi watakapokumbwa na magonjwa, shabaha ya Serikali ikiwa ni kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na uhakika wa huduma bora za matibabu.

Mkutano huu unawakutanisha wataalam mbalimbali wa Sekta ya Afya kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na wadau wa maendeleo ikiwa ni maandalizi ya Mkutano Mkuu utakaofanyika Machi 30, 2026.