Ministry of Health

TANZANIA,KOREA KUIMARISHA MAABARA YA TAIFA KUDHIBITI MAGONJWA YA KUAMBUKIZA

Posted on: May 7th, 2026



Wizara ya Afya kupitia Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (NPHL), kwa kushirikiana na Shirika la Korean Foundation for International Healthcare (KOFIH), imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha uwezo wa Watumishi wa Maabara nchini katika kudhibiti na kusimamia magonjwa ya mlipuko. hatua hii inafanywa kupitia utekelezaji wa mradi wa miaka mitano (2023-2027) unaofadhiliwa kwa ushirikiano na KOFIH.

Hayo yamebainishwa leo, tarehe 7 Mei 2026,Jijini Dar es salaam na Dkt. Medard Beyanga, akimwakilisha Mkurugenzi wa uchunguzi na vifaa tiba kutoka Wizara ya Afya, wakati wa Kikao cha Usimamizi wa Mradi wa Kujengea Uwezo Watumishi wa Maabara ya Taifa katika Menejimenti ya Magonjwa ya Kuambukiza.

Dkt. Beyanga amesema, mradi huu umejikita katika kuongeza uwezo wa wataalamu wa maabara katika maeneo ya utambuzi, ufuatiliaji, na uchambuzi wa magonjwa mbalimbali ya kuambukiza, ikiwemo dengue, chikungunya, kipindupindu, pamoja na magonjwa ya njia ya hewa.

Aidha,Dkt.Beyanga amesisitiza kuwa, mradi huo umewezesha kuimarishwa kwa uchunguzi wa vinasaba vya vimelea vinavyosababisha magonjwa hayo hapa nchini.

Ameongeza kuwa, Wataalamu wa Maabara wamepata nafasi ya kufanya tathmini ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa mradi huo, sambamba na kujadili changamoto zinazoweza kujitokeza katika usimamizi wa magonjwa ya kuambukiza nchini. Amebainisha hatua hiyo inalenga kuhakikisha mfumo wa maabara nchini unaendelea kuwa imara na kuwa na uwezo wa kutoa majibu sahihi kwa wakati.

Dkt. Beyanga ameeleza kuwa, kuimarishwa kwa uwezo wa Maabara ya Taifa ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa ajenda ya Serikali ya kuboresha sekta ya afya nchini, hasa katika kipindi ambacho dunia inaendelea kukabiliwa na changamoto za magonjwa ya mlipuko na ya kuambukiza.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Korean Foundation for International Healthcare (KOFIH, Dkt. Hansol Park amesema mradi huo unalenga kuimarisha mifumo ya uchunguzi na ufuatiliaji wa magonjwa kama dengue, kipindupindu, na magonjwa mapya ya mfumo wa hewa.