TANZANIA YATANGAZA FURSA MPYA ZA UWEKEZAJI SEKTA YA AFYA KIMATAIFA
Posted on: March 18th, 2026Na WAF, London
Tanzania imetangaza kuwa iko tayari kushirikiana na wawekezaji wa kimataifa katika kukuza sekta ya afya na sayansi, ikiwa na lengo la kuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya barani Afrika.
Akizungumza jijini London kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia dawa na vifaa tiba, Emmanuel Tayari, amesema Serikali imejizatiti kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa uwekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba.
Amesema juhudi hizo zinaungwa mkono na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, huku Serikali ikiiona sekta ya afya kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi, si huduma ya kijamii pekee. Lengo ni kuimarisha uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, hasa baada ya uzoefu wa UVIKO-19.
Ikiwa na zaidi ya watu milioni 65 pamoja na soko la kikanda kupitia EAC na SADC, Tanzania inaendelea kuvutia uwekezaji katika uzalishaji, usambazaji na ubunifu wa huduma za afya.
Serikali pia inaendelea kuendeleza maeneo maalum ya uwekezaji kama Mloganzila na Kibaha, pamoja na kurahisisha taratibu kupitia mifumo maalum ili kuharakisha uwekezaji wa kimkakati.
Aidha, imesisitiza uzalishaji wa dawa bora zinazokidhi viwango vya kimataifa, huku ikiwaonya wawekezaji dhidi ya bidhaa duni au teknolojia zilizopitwa na wakati.