Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TANZANIA YANG'ARA HUDUMA ZA MAABARA AFRIKA

Posted on: May 24th, 2024



Na, WAF - DODOMA

Tanzania imekuwa nchi ya tatu kwa ubora wa Huduma za maabara kati ya nchi 56 za Bara la Afrika kupata ithabati ya ubora.

Hayo yameelezwa Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, leo Mei 24, 2024Jijini Dodoma wakati wa hafla ya ugawaji wa vyeti kwa maabara zilizopata idhibati ya Kimataifa.

"Tuna kila sababu ya kujipongeza hili ni jambo kubwa, nawapongeza mmefanya jambo kubwa sisi kama Serikali tunajivunia ninyi wataalamu wa maabara," amesema Dkt. Mollel

Amesema anaamini mwakani watakuwa nafasi ya kwanza, kwani Rais Samia Suluhu Hassan amezidi kutoa fedha katika sekta ya afya ili wananchi waweze kupata Huduma bora na za wakika.

Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha watu wa maabara wanaendelea kuwa na maslahi na kuwataka wataalamu hao kujiamini na kufanya vizuri zaidi katika kutoa Huduma bora za maabara.

"Natoa rai kwa wasimamizi wa Hospitali kuhakikisha wanawawezesha watu wa maabara, naombeni mnaofanya maamuzi kwenye eneo la maabara hili liangalieni hawa ni watu muhimu sana katika hospitali zetu nchini.

Aidha amewatia moyo wataalamu hao na kuwambia wasibweteke kwani Serikali chini ya Uongozi wa Rais Samia umewekeza vifaa na miundombinu ya kisasa ili mwananchi aweze kupata Huduma bora za afya.

Vile vile Dkt. Mollel ameagiza vituo vya afya kutumia miongozo katika kuboresha huduma za maabara na serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kusimamia afua za uboreshaji wa huduma za afya nchini.

"Hivyo nitoe rai kwa viongozi wote tuweze kusimamia kikamilifu vituo ili vitumie miongozo yote iliyotolewa na Wizara ya Afya katika kuboresha huduma zetu za Maabara nchini kwa ubora wenye kiwango cha kimataifa,"amesisitiza Dkt. Mollel.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Ubora na Uchunguzi wa Magonjwa na Matengenezo ya vifaa tiba, Dkt. Alex Magesa amesema lengo la Mkutano huo ni kutoa tuzo na vyeti kwa maabara zilizopata ithibati za kimataifa kwa mwaka wa fedha 2023-2024.

Dkt. Magesa amesema wadau wa maabara wanashirikana katika kuboresha sekta ya maabara lengo likiwa ni kuhakikisha huduma bora na nzuri zinatolewa