Ministry of Health

TANZANIA YAIBUA FURSA KUBWA UWEKEZAJI DAWA MAONESHO YA CPHI CHINA

Posted on: June 17th, 2026

Tanzania imeendelea kujiweka katika nafasi ya kimkakati ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa barani Afrika baada ya kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Dawa ya CPHI China 2026 yanayofanyika jijini Shanghai kuanzia Juni 16 hadi 18, 2026.

Ushiriki huo unafanywa na Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji wa Sekta ya Dawa na Vifaa Tiba (PIAT), ambacho kimewasili nchini China kwa dhamira ya kutangaza fursa za uwekezaji na kuvutia wazalishaji wakubwa wa dawa duniani.

Ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari, ukiwa na lengo la kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na wazalishaji wa dawa, malighafi za dawa (APIs), pamoja na kampuni za uzalishaji wa dawa kwa mikataba.

Akizungumza leo Juni 17, 2026 jijini Changai Tayari amesema kupitia majadiliano hayo, Tanzania inawasilisha kwa wawekezaji uwezo wake mkubwa wa kuwa kitovu kipya cha uzalishaji wa dawa kwa ajili ya soko la ndani na la kikanda.

Maonesho ya CPHI China yanatajwa kuwa miongoni mwa majukwaa makubwa zaidi ya biashara ya dawa barani Asia, yakikusanya wadau kutoka mataifa mbalimbali duniani.

"Ushiriki wa Tanzania katika jukwaa hilo unaipa nchi fursa adhimu ya kujitangaza mbele ya wawekezaji wenye uwezo wa kuanzisha viwanda vikubwa vya dawa na kuongeza upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya barani Afrika", amesema Naibu Katibu Mkuu Tayari.

Katika siku za mwanzo za maonesho hayo, banda la Tanzania limevutia idadi kubwa ya wawekezaji waliodhihirisha nia ya kushirikiana katika uwekezaji wa viwanda vya dawa, chanjo, bidhaa za kibaolojia, dawa za sindano na uzalishaji wa malighafi za dawa.

Bw. Tayari amesema Tanzania imeendelea kuonesha mageuzi makubwa yanayofanyika katika sekta ya afya na viwanda vya dawa, ikiwemo kuboresha mifumo ya udhibiti, kutoa vivutio vya uwekezaji, kuimarisha ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na kuanzisha maeneo maalum ya viwanda vya dawa