Ministry of Health

TANZANIA YAAHIDI KUONGEZA MCHANGO KATIKA JUHUDI ZA KUDHIBITI UGONJWA WA EBOLA AFRIKA

Posted on: June 16th, 2026

Na Clement Robert, WAF - Dodoma

Tanzania imeeleza utayari wake wa kuunga mkono juhudi za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda kwa kutoa vifaa tiba, vifaa kinga kwa wahudumu wa afya pamoja na wataalamu wenye uzoefu katika kudhibiti milipuko ya magonjwa.

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 16,2026 na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na wadau uliojadili hatua za kukabiliana na mlipuko wa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo katika nchi hizo mbili.

Amesema, Tanzania imeeleza mshikamano wake na serikali pamoja na wananchi wa DRC na Uganda, huku ikitoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao kutokana na ugonjwa huo na kuwatakia nafuu ya haraka wagonjwa wote walioathirika.

“Tanzania tumeendelea kuimarisha uwezo wa kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa kupitia uwekezaji katika mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, uchunguzi katika maeneo ya mipakani, maabara, vifaa tiba na mifumo ya mwitikio wa haraka, huku tukijidhatiti na kuhimiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda na bara zima”

Mhe. Mchengerwa ameongeza, kwa kuitaka Africa CDC pamoja na nchi wanachama kuimarisha zaidi uratibu, kuwekeza katika mifumo ya maandalizi na mwitikio wa haraka, na kuhakikisha rasilimali zinapatikana kwa wakati ili kudhibiti mlipuko wa sasa, kuzuia majanga yajayo na kujenga Afrika yenye afya na usalama zaidi.
 
Aidha, Tanzania imepongeza juhudi za Rais wa Burundi, Mheshimiwa Ndayishimiye, Tume ya Umoja wa Afrika, Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa uratibu na uongozi wao katika kuitisha mkutano huo na kusimamia hatua za mwitikio dhidi ya mlipuko huo.