Customer Feedback Centre

Ministry of Health

AFUA ZA MPOX KUZIDI KUIMARISHWA NCHINI

Posted on: September 3rd, 2024

Na WAF, Dodoma


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha zaidi afua za kinga na utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Mpox endapo ugonjwa huo utaingia nchini kwani hadi sasa hakuna mgonjwa aliethibitika kuwa na maambukizi nchini.


Dkt.  Mollel ameyasema hayo leo Septemba 04, 2024 kwa Niaba ya Waziri wa Afya Mhe Jenista Mhagama wakati akichangia katika Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa afya wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya mtandao akiwa jijini Dodoma.


Dkt. Mollel amesema Tanzania imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuimarisha uchunguzi kwa wasafiri kupitia huduma za Afya Mipakani,bandari, nchi kavu na viwanja vya ndege ili kubaini wasafiri wenye viashiria na dalili za ugonjwa huu na kuchukua hatua stahiki. 


“Tunaendelea kutoa mafunzo elekezi kwa watumishi mbalimbali juu ya utambuzi wa ugonjwa wa Mpox  kujikinga na kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya Mpox, elimu ya Mpox kwa umma inaendelea ili kuhamasisha jamii kuchukua tahadhari na kujikinga dhidi ya Mpox kupitia vipeperushi, vyombo vya habari, nyumba za ibada, masoko na minada.” Amesema Dkt. Mollel 


Pia, Dkt. Mollel amesisitiza juu ya umuhimu wa kuimarisha afua za WASH hususani kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka ili kupunguza uwezekano wa kupata na kusambaza maambukizi ya Mpox.


“Kwa kuwa ugonjwa huu unaambukizwa kwa kugusana, Wizara inaweka mkazo kwa jamii kunawa mikono kila mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono hivyo tumetoa wito kwa maeneo ya umma, kaya na taasisi mbalimbali ikiwemo shule, vyuo na vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha kunakuwa na vifaa vya kunawia mikono vyenye maji tiririka na sabuni ili kurahisisha unawaji wa mikono.” Amesisitiza


Aidha, ameongeza kuwa Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania tayari imeandaa na kusambaza miongozo na nyaraka mbalimbali za Mpox, ikiwemo Mpango Mkakati wa Utayari wa Kukabiliana na Mpox, miongozo hiyo inaendelea kutumika ili kuimarisha utayari kuboreshwa kadri hali ya ugonjwa inavyolazimu. 


Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu katibu Mkuu Bw. Ismail Rumatila pamoja na wajumbe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya mambo ya Ndani na Jeshi la Uhamiaji