Ministry of Health

TANZANIA, INDIA KUHAKIKISHA MIFUMO YA TIBA ASILI, KISASA KUSOMANA 2030

Posted on: March 26th, 2026

Na. Aisha Swahibu, WAF - Dodoma

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini makubaliano na nchi ya India yenye lengo la kuhakikisha mifumo ya tiba asili na tiba ya kisasa inaunganishwa kuanzia ngazi ya afya ya msingi ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, leo Machi 25, 2026, wakati wa kikao chake na wataalamu wa tiba asili kilichofanyika jijini Dodoma, chenye kauli mbiu isemayo: “Kuimarisha huduma za tiba asili zenye ushahidi wa kisayansi.”

Mhe. Mchengerwa amesema kuwa kasi ya utekelezaji inapaswa kuongezwa ili kufikia malengo yaliyowekwa, akisisitiza kuwa Tanzania ina nafasi kubwa ya kuwa kinara katika matumizi ya tiba asili.

“Nikiwa kwenye Ziara nchini India, shirika la afya duniani (WHO) kuna mataifa yanayotambuliwa kwa matumizi ya tiba asili licha ya kuwa hayajafikia hata nusu ya hatua iliyofikiwa na Tanzania. Hivyo, tunahitaji kuongeza umakini na kasi ya utekelezaji ili tusipitwe na wengine,” amesema Mhe. Mchengerwa

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema Wizara ya Afya imepanga kutenga fungu maalum katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kutoa msaada kwa wataalamu wa tiba asili, hatua itakayosaidia kukuza sekta hiyo na kuwawezesha wataalamu kuboresha huduma zao.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kujenga uchumi unaojitegemea kupitia viwanda vya uzalishaji dawa, amesema katika eneo la Hospitali ya Mloganzila kuna uwezekano wa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wataalamu wa tiba asili kuanzisha viwanda vyao vya uzalishaji wa dawa.