Ministry of Health

TANZANIA, CHINA WAFIKIA MUAFAKA WA MAKUBALIANO YA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Posted on: May 31st, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF - Kagera

Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China zimefikia muafaka wa kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya kwa lengo la kuboresha huduma za tiba, tafiti, mafunzo ya wataalamu wa afya na uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amesema hayo leo Mei 30, 2026 ambapo makubaliano hayo yametokana na mazungumzo yaliyofanyika kati ya Waziri wa Afya wa Tanzania Bara Mhe. Mohammed Mchengerwa na Waziri wa Afya wa Jamhuri ya watu wa China Mhe. Haichao Lei wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHA) uliofanyika Geneva, Uswisi.

"Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China tumekubaliana wataalamu wetu waandae andiko dhana na mpango wa utekelezaji kwa kuanzia na uboreshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera pamoja na utanuzi wa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto JKCI, makubaliano haya yatasaidia uboreshwaji wa huduma kwa wananchi," amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema maeneo makuu ya ushirikiano ni pamoja na kuimarisha huduma za rufaa katika Hospitali ya Mkoa ya Kagera, mapambano dhidi ya magonjwa ya milipuko, kuboresha huduma za matibabu na upasuaji wa moyo kwa watoto pamoja na mafunzo ya watumishi wa Afya katika nyanja za tiba, tafiti na ubunifu.

Pia, Dkt. Magembe amesema pande hizo mbili zimekubaliana kuwezesha wataalamu wa afya kutoka Tanzania kwenda China kwa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu, huku wataalamu kutoka China nao wakija nchini kubadilishana uzoefu na ujuzi.

Mwisho, Dkt. Magembe ameishukuru Serikali kwa kudumisha mashirikiano mazuri na mataifa mengine pamoja na Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa kuwezesha ziara ambayo imeibua fursa za ushirikiano huo wenye manufaa kwa maendeleo ya sekta ya afya nchini.