Ministry of Health

TAASISI ZA AFYA ZAPEWA NGUVU MPYA KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI

Posted on: March 27th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Dodoma

Wizara ya Afya imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuziimarisha taasisi zake ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha sekta hiyo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Machi 26, 2026 jijini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI.
Amesema Serikali imeendelea kuziimarisha taasisi zake ikiwemo Bohari ya Dawa (MSD), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) pamoja na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ili kuhakikisha zinatimiza majukumu yake kwa ufanisi.

Katika kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, Serikali imewekeza katika Bohari ya Dawa kwa kuboresha miundombinu ya uhifadhi ikiwemo ujenzi wa maghala makubwa, hatua inayolenga kuimarisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali imeendelea kuimarisha huduma za bima ya afya kupitia NHIF, pamoja na kulipa sehemu ya madeni yaliyokuwa yanaiathiri taasisi hiyo, ili kuongeza uwezo wa wananchi kupata huduma za matibabu bila vikwazo vya kifedha.

Kwa upande wa udhibiti wa ubora wa dawa na vifaa tiba, Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa TMDA katika kusimamia usalama na ubora wa bidhaa hizo, huku NIMR ikiendelea kufanya tafiti mbalimbali zinazosaidia kuboresha sera na mipango ya afya nchini.

“Tunaziimarisha taasisi hizi ili ziweze kuwa nguzo imara katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi,” amesema Mhe. Mchengerwa.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika taasisi hizo kwa kuongeza rasilimali, kuimarisha mifumo ya TEHAMA pamoja na kujenga uwezo wa wataalam ili kukidhi mahitaji ya sekta ya afya inayoendelea kukua kwa kasi kubwa katika utawala wa Serikali ya awamu ya Sita