Ministry of Health

STUDIO MPYA YA JKCI KUBORESHA ELIMU YA AFYA YA MOYO KWA WANANCHI

Posted on: June 12th, 2026

Na Atley Kuni, WAF – Dar es Salaam

Serikali imesema JKCI Health Promotion Studio, ni kituo maalumu cha utoaji wa elimu ya afya kwa umma kilichopo katika Jengo jipya la Utawala na Vipimo la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), hatua inayolenga kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe Mohamed Mchengerwa wakati wa uzinduzi huo Juni 12, 2026.

Waziri Mchengerwa, amesema studio hiyo ni sehemu ya uwekezaji wa kimkakati wa Serikali katika kuzuia magonjwa kabla hayajaleta madhara makubwa kwa wananchi.

Amebainisha kuwa magonjwa mengi yasiyoambukiza, yakiwemo shinikizo la damu, kisukari na baadhi ya magonjwa ya moyo, yanaweza kuzuilika kupitia elimu sahihi na mabadiliko ya mtindo wa maisha.

"Studio hiyo itatumika kuzalisha na kusambaza taarifa za afya ya moyo kwa wananchi kupitia njia mbalimbali za mawasiliano, ikiwemo redio, televisheni, mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha ujumbe wa afya unawafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati na kwa lugha rahisi kueleweka.

Amefafanua kuwa kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza duniani kunahitaji uwekezaji mkubwa wa elimu ya afya kwa umma ili kuwajengea wananchi uwezo wa kutambua vihatarishi vya magonjwa hayo na kuchukua hatua za kujikinga mapema.

Mchengerwa ameongeza kuwa studio hiyo itasaidia kubadilisha mtazamo wa mfumo wa afya kutoka kwenye tiba pekee kwenda kwenye kinga, jambo ambalo linaweza kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi na Serikali kwa ujumla. Tafiti

Mbali na kutoa elimu kwa wananchi, studio hiyo pia itatumika kama jukwaa la wataalamu wa afya kutoa ushauri, kujibu maswali ya wananchi na kuendesha kampeni za uhamasishaji kuhusu afya ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza.

"Uwepo wa studio hii unatarajiwa kuimarisha nafasi ya JKCI kama taasisi inayoongoza si tu katika matibabu ya moyo, bali pia katika utoaji wa elimu na uhamasishaji wa afya kwa jamii. Kupitia maudhui yatakayozalishwa, wananchi watapata maarifa yatakayowawezesha kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya zao na kupunguza hatari ya kupata magonjwa yanayozuilika.