Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SHAHADA YA SAYANSI YA MAZOEZI TIBA KUBORESHA HUDUMA ZA UTENGAMAO

Posted on: April 28th, 2024


Na WAF - Dar Es Salaam


Serikali kupitia Wizara ya Afya ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS) imeanzisha Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Mazoezi Tiba ili kusaidia mawasiliano (Speech pathology), Tiba Kazi (Occupational therapy) na Tiba Viungo (Physiotherapy) kuanzia mwaka 2024 ili kuboresha huduma za utengamao.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Muwalimu amesema hayo leo Aprili 28, 2024 baada ya mbio za ‘Run4Autism’ (watoto wenye Usonji) za KM 5 zilizoanzia katika viwanja vya farasi kupitia daraja la Tanzanite Jijini Dar Es Salaam zikiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa. 


“Tumeanzisha na shahada ya kwanza ya Sayansi ya Saikolojia ya Kitabibu (Clinical Psychology) kuanzia mwaka huu wa 2024 lengo likiwa ni kuhakikisha huduma za utengemao zinapewa kipaumbele cha juu na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan”. Amesema Waziri Ummy 


Waziri Ummy amesema, Serikali inaendelea kufanya juhudi za kutatua changamoto za watu wenye Usonji ambapo amebainisha miongoni mwa changamoto hizo hi pamoja na upungufu wa wataalam wa mazoezi tiba pamoja na gharama za mazoezi tiba kwa watu wenye Usonji. 


“Tunategemea pia kuanzisha fani hizi katika ngazi Diploma kwa Mwaka wa fedha 2024/25 kwa kuwa nchi ni kubwa ili tuweze kuwa na watalaam wengi zaidi wa masuala ya ‘Speech pathology’, ‘Occupational therapy’, ‘Physiotherapy’ katika ngazi za vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya kote nchini.


Kwa upande wake Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Lukiza Autism Tanzania Bi. Hilda Nkabe ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuona umuhimu wa kuanzisha Shahada hizo. 


“Tunashukuru sana Serikali kwa kutuunga Mkono kwenye Taasisi yetu pamoja na kutambua watu wenye Usonji, tunaomba Serikali iendelee kuwapa kipaumbele hasa kwenye elimu pamoja na kazi za ufundi ambazo pia zinaweza kufanywa na watu wenye Usonji.” Amesema Bi. Nkabe.