Ministry of Health

SERIKALI YAWEKA MKAZO KWA WATAALAM WA TIBA ASILI KUJISAJILI

Posted on: April 8th, 2026

Na Zakayo Mosha, WAF – Tabora

Serikali imewataka wataalam wa tiba asili na tiba mbadala nchini kujisajili rasmi na kuzingatia maadili ya taaluma, huku ikionya kuwa wale watakaoendelea kutoa huduma bila usajili halali watachukuliwa hatua za kisheria.

Wito huo umetolewa Aprili 8, 2026 mkoani Tabora na Msajili wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Lucy Mziray, alipofika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kukutana na Mganga Mkuu wa Mkoa pamoja na wataalam wa sekta ya afya. Amesema zoezi la kuhamasisha na kusajili papo kwa papo linaenda sambamba na utoaji wa elimu ya huduma salama, ikiwemo kujikinga na maambukizi ya magonjwa mbalimbali.

“Hatua hii inalenga kuwatambua wataalam halali waliopo katika jamii na kudhibiti matapeli wanaojipenyeza kwenye sekta hii kwa lengo la kujipatia kipato kinyume cha sheria,” amesema Mziray, akiongeza kuwa Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa maeneo yenye wataalam wengi wa tiba asili, ingawa wengi wao bado hawajajisajili na wanaendesha shughuli zao kienyeji.

Amefafanua kuwa Wizara ya Afya imeanzisha kampeni ya uhamasishaji katika halmashauri zote nane za mkoa huo kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma hizo. Kwa mujibu wa ratiba, zoezi hilo litafanyika Kaliua Aprili 9–10, Urambo Aprili 11–12, Sikonge Aprili 14–15, Uyui Aprili 16–18, Igunga Aprili 20–21, Nzega DC Aprili 22–23, Nzega TC Aprili 24–25 na kumalizika katika Manispaa ya Tabora Aprili 27–28, 2026. Wanaojisajili kwa mara ya kwanza wanapaswa kuwa na barua ya utambulisho kutoka Serikali ya Kijiji, mtaa au kata, muhtasari wa kikao cha kuwatambua pamoja na kitambulisho cha mpiga kura au NIDA.

“Tunawaomba wataalam wa tiba asili na tiba mbadala kutumia fursa hii kufika katika maeneo husika kupata elimu na kusajiliwa papo kwa papo, iwe ni kwa wanaojisajili kwa mara ya kwanza au wanaohuisha taarifa zao za kila mwaka,” amesema Mziray.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Honoratha Rutatinisibwa, ameipongeza Serikali kwa kuwasogezea huduma hiyo karibu wananchi kupitia halmashauri, hatua inayopunguza gharama kwa wataalam hao. Amesema bado kuna baadhi ya watoa huduma wanaofanya kazi bila usajili na kusababisha upotoshaji