Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI YAWEKA MKAKATI KUBORESHA UTOAJI ELIMU, HUDUMA ZA AFYA

Posted on: June 8th, 2025

Na WAF, Dodoma

Katika juhudi za kuimarisha elimu ya afya kwa umma na huduma za afya ngazi ya jamii nchini, Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI imefanya mkutano wa kitaifa wa waratibu wa elimu ya afya kutoka mikoa yote 26 na halmashauri 184.

Mkutano huo uliofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma, umefunguliwa Juni 6, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Otilia Gowelle ambaye ameeleza kuwa utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs) unalenga kuongeza ufanisi wa utoaji wa elimu ya afya.

Ameeleza kuwa lengo lingine kuwa ni uhamasishaji wa jamii na upatikanaji wa huduma bora katika maeneo ya vijijini na mijini kwa kuzingatia vipaumbele vya kiafya vya kitaifa.

Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni.pamoja na afya ya uzazi, magonjwa ya mlipuko, lishe, magonjwa yasiyo ya kuambukiza na chanjo.

"Mkutano huu utaweka mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa afua za uelimishaji kupitia Mpango Jumuishi wa CHWs," amefafanua Dkt. Gowelle.

Mkutano huo pia umejadili kwa kina majukumu na hadidu za rejea za waratibu wa elimu ya afya ngazi ya mkoa na wilaya, na kuweka mfumo wa uratibu, ufuatiliaji na tathmini wa pamoja utakaosaidia kufanikisha utekelezaji wa shughuli zote za elimu ya afya, ikiwemo usimamizi wa CHWs, elimu mashuleni, mabadiliko ya kitabia.

Kwa upande wao, waratibu wa mikoa na halmashauri walipata nafasi ya kuwasilisha mikakati yao ya utekelezaji, changamoto zinazowakabili, na mapendekezo ya kuboresha uratibu wa elimu ya afya kwa umma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Mkutano huo uliohitimishwa Juni 7, 2025 umeweka msingi thabiti wa kuunganisha juhudi za Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa na jamii katika kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na elimu sahihi ya afya na huduma zinazohitajika kwa wakati.