Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI YAWEKA MIPANGO YA TATHMINI CHUO KIPYA UKEREWE

Posted on: May 29th, 2025

Na, WAF-Dodoma.


Serikali imethibitisha kuwa bado kuna mahitaji ya uanzishwaji wa vyuo vya uuguzi na uganga katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwa ni pamoja na wilaya ya Ukerewe ambapo kwa sasa juhudi zimeelekezwa kwenye ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa katika wilaya hiyo.


Akijibu swali la Mbunge wa Ukerewe, Mhe. Joseph Michael Mkundi,  leo Mei 29, 2025 Bungeni Jijini Dodoma, alilyetaka kufahamu ni lini Serikali itajenga tawi la Chuo cha Uuguzi na Uganga Ukerewe, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa Serikali itaendelea kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini kama kuna uhitaji wa kuanzisha Chuo cha Uuguzi katika eneo hilo, mara baada ya kukamilika kwa hospitali hiyo.


“Ni kweli bado kuna mahitaji ya vyuo katika maeneo mbalimbali ya nchi, ila kwa sasa Serikali inajenga hospitali yenye hadhi ya Rufaa ya Mkoa katika wilaya ya Ukerewe. Sambamba na ujenzi huo, Serikali itaendelea kufanya upembuzi yakinifu kuona kama eneo hilo litahitaji kuwa na Chuo cha Uuguzi,” amesema Dkt. Mollel.


Katika swali la nyongeza, Mhe. Mkundi amehoji iwapo Serikali haioni haja ya kutumia majengo ya zamani ya halmashauri yaliyoachwa baada ya ujenzi wa majengo mapya, kwa ajili ya kuanzisha chuo hicho, Dkt. Mollel amesema "Wizara itatuma timu ya wataalam kwenda Ukerewe kwa ajili ya kufanya tathmini (survey) na kuangalia kama majengo hayo yanakidhi vigezo vya kutumika kama chuo cha afya.


Hata hivyo, Dkt. Mollel amesisitiza kuwa uwepo wa chuo cha afya unahitaji hospitali ya karibu itakayoweza kutumika kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi kwakuwa hii ni sababu mojawapo ya kusubiri kukamilika kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ili kuhakikisha mazingira bora ya kujifunzia yanapatikana.



Uamuzi wa Serikali kufanya tathmini zaidi unaonesha dhamira ya kuhakikisha kuwa rasilimali na miundombinu vinatumika kwa ufanisi, sambamba na kukidhi mahitaji halisi ya huduma za afya na mafunzo kwa watumishi wa sekta hiyo.