Ministry of Health

SERIKALI YASEMA TIBA ASILI KUWA NGUZO YA VIWANDA VYA DAWA NA UCHUMI WA TAIFA

Posted on: March 25th, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF - Dodoma


Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema mustakabali wa tiba asili nchini haupaswi kubaki pembezoni mwa mfumo wa afya na uchumi, bali uwe sehemu ya mkakati mpana wa taifa wa kujenga viwanda vya dawa, kuongeza ajira, kukuza utafiti, kulinda maarifa ya jadi na kupanua wigo wa mchango wa sekta ya afya na pato la taifa.


Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo, Machi 25, 2026, wakati wa mkutano wake na wataalamu wa tiba asili uliofanyika jijini Dodoma, ukiwa na kauli mbiu: “Tuimarishe huduma za tiba asili zenye ushahidi wa kisayansi.”


"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda, kuimarisha uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya Nchi," amesema Mchengerwa na kuongeza.


“Katika muktadha huo, sekta ya dawa ni eneo la kimkakati sana. Tunahitaji kuwa na uwezo wa kuzalisha dawa zetu hapa nchini kwa ubora unaokubalika, kwa usalama unaothibitika, na kwa ushindani utakaoiwezesha Tanzania kuhudumia soko la ndani, kikanda na kimataifa,” amesema Mhe. Mchengerwa.


Aidha Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa dhana ya viwanda vya dawa haipaswi kuishia kwenye dawa za kisasa pekee, bali ijumuishe pia dawa, virutubisho na bidhaa tiba zitokanazo na rasilimali za tiba asili ambazo Tanzania imejaliwa kwa wingi.


“Nchi yetu ina utajiri mkubwa wa bioanuwai, maarifa ya jadi na uzoefu wa watoa huduma wa tiba asili uliojengwa kwa vizazi vingi,” amesema.


Mhe. Mchengerwa amefafanua kwamba, tiba asili ni mtaji mkubwa wa kitaifa ambao haupaswi kubaki katika uzalishaji mdogo usio na thamani kubwa ya kiuchumi. Badala yake, inapaswa kugeuzwa kuwa nguvu ya uzalishaji, ubunifu, biashara na ajira kupitia mfumo rasmi, salama na wenye tija.