SERIKALI YAONGEZA TAHADHARI DHIDI YA EBOLA, YASISITIZA WANANCHI KUCHUKUA HATUA
Posted on: May 19th, 2026Na Atley Kuni, WAF-Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imewahakikishia wananchi kuwa hadi sasa Tanzania haina kisa chochote cha ugonjwa wa Ebola, huku ikiendelea kuimarisha hatua za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo baada ya nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda kuripoti mlipuko wa Ebola.
Akitoa taarifa kwa umma mjini Dodoma Mei 18, 2026, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini kutokana na mwingiliano mkubwa wa kijamii na kiuchumi uliopo kati ya Tanzania na nchi zilizoathirika.
Dkt. Magembe amesema Ebola husababishwa na virusi vinavyoenea kutoka kwa popo na wanyama jamii ya sokwe kwenda kwa binadamu, na baadaye kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia majimaji ya mwili wa mgonjwa au mtu aliyefariki kwa ugonjwa huo.
Amesema dalili za Ebola ni pamoja na homa, uchovu wa mwili, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa, kutapika na kuharisha. Baadhi ya wagonjwa wanaweza kupata vipele pamoja na kutokwa damu sehemu mbalimbali za mwili kama macho, pua, masikio na mdomo.
"Serikali imeendelea kuimarisha uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaoingia nchini kupitia mipaka, bandari na viwanja vya ndege ili kubaini mapema viashiria vya ugonjwa huo" amesema Dkt. Magembe na kuongeza
"Serikali pia imepeleka wataalam katika mikoa yenye hatari kubwa na kuhakikisha vituo vya afya vina dawa, vifaa kinga na huduma muhimu za kukabiliana na Ebola endapo ugonjwa utaingia nchini" amesisitiza Dkt. Magembe
Wizara ya Afya imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia televisheni, redio na mitandao ya kijamii kuhusu njia za kujikinga na ugonjwa huo. Serikali pia imeimarisha ushirikiano na nchi jirani pamoja na kuhuisha mwongozo wa wasafiri kuanzia Mei 19, 2026 kwa mujibu wa Kanuni za Afya za Kimataifa.
Dkt. Magembe amewataka wananchi kuendelea kuzingatia kanuni za afya ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka kugusa majimaji ya mwili ya mtu mwenye dalili za Ebola, na kuwahi hospitali endapo watapata dalili zinazofanana na ugonjwa huo.