Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI YAIMARISHA UTAYARI WA MIKOA 11 KUKABILIANA NA MATUKIO YA DHARURA ZA AFYA YA JAMII

Posted on: August 24th, 2023

Na. Majid Abdulkarim, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kujiimarisha katika utayari wa kukabiliana na Matukio ya dharura ya afya ya jamii, magonjwa ya mlipuko na Matukio yenye adhari za afya ya jamii kwa kutoa mafunzo elekezi kwa Waratibu wa Mikoa wa vituo vya uratibu Matukio ya dharura za afya ya jamii (PHEOC)

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe wakati akifungua mafunzo ya Waratibu wa Mikoa wa vituo vya uratibu Matukio ya dharura za afya ya jamii, pamoja na Waratibu wa ufuatiliaji wa magonjwa na Matukio yenye athari za afya ya jamii.

Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha watanzania wanakuwa salama na afya bora ili kufanya shughuli zao za kiuchumi na kujenga taifa kwa ujumla.

Aidha Dkt. Magembe amesema kujengewa uwezo kwa wataalam hao kutasaidia kuharakisha uchakataji wa taarifa na kuchukua hatua madhubuti na za haraka za udhibiti wa matukio hayo.

Ameeleza kuwa mikoa hiyo 11 ni mikoa ya awali ya kipaumbele kutokana na uwezekano wa kupata dharura mbalimbali kama magonjwa ya mlipuko kutokana na jiografia na mwingiliano wa kiuchumi katika Mikoa hiyo.

“Mikoa na Halmashauri ni ngazi muhimu katika kuleta mabadiliko (game changer) kwenye udhibiti wa matukio ya dharura ya afya ya jamii ikiwemo magonjwa ya milipuko”. Amesema Dkt. Magembe.

Kwa kuongezea amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mikakati ya kukabiliana na magonjwa ya dharura ikiwemo magonjwa ya mlipuko na ajali mbalimbali.

Mafunzo hayo yamejumuisha waratibu kutoka mikoa 11 kutoka Tanzania bara na visiwani chini ya ufadhili wa Kituo cha kukinga na kudhibiti Magonjwa cha Afrika (Africa CDC), Marekani (US CDC) na Shirika la Afya Duniani.

Dkt. Magembe amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu mikakati iliyowekwa na serikali ili kuhakikisha wanailinda nchi na majanga, maafa ikiwemo magojwa ya mlipuko na ajali.

Pia Dkt. Grace amesema hivi karibuni Tanzania ilifanyiwa tathmini na Dunia kuona utayari wa kukabiliana na dharura za magonjwa ya mlipuko, maafa na majanga.