SERIKALI YAENDELEA KUSIMAMIA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA LINDI
Posted on: May 12th, 2026Na. Aisha Swahibu, WAF - Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi unaotekelezwa kwa awamu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi na maeneo jirani.
Hayo amesema Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi leo Mei 13, 2026, bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini Mhe. Mohamed Musa Utaly alipouliza Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi ?,
Dkt. Samizi amesema kuwa awamu ya kwanza na ya pili ya mradi huo tayari zimekamilika kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 4. Kupitia utekelezaji huo, sakafu ya kwanza ya hospitali imekamilika na tayari inaendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha, Dkt. Samizi ameeleza kuwa Wizara ya Afya imeingia mkataba kwa ajili ya ukamilishaji wa awamu ya tatu ya ujenzi huo ambapo mkandarasi alianza rasmi kazi mwezi Novemba, 2025 kwa mkataba wa miezi 12, ujenzi huo unatarajiwa kukamilika kabla au ifikapo mwezi Desemba, 2026.
Katika hatua za utekelezaji wa mradi huo, Dkt. Samizi amesisitiza kuwa mpaka sasa mkandarasi amelipwa kiasi cha shilingi milioni 812 kama hati ya malipo ya awali (advance payment) ili kuwezesha kuendelea kwa kazi za ujenzi kwa mujibu wa mkataba.
Mwisho, ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kufuatilia na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, hatua itakayochangia kuimarika kwa huduma za afya katika Mkoa wa Lindi na maeneo ya jirani.