Ministry of Health

SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA UCHUNGUZI WA KIFUA KIKUU KUPITIA HUDUMA ZA MAABARA

Posted on: June 10th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Morogoro

Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP), kwa kushirikiana na CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, imeendelea kuimarisha huduma za maabara za kifua kikuu nchini kwa lengo la kuongeza uwezo wa kugundua ugonjwa huo mapema, kuboresha ubora wa vipimo na kuimarisha udhibiti wake.

Hayo yameelezwa leo Juni 10, 2026 na Mkuu wa Maabara Kuu ya Kifua Kikuu, Dkt. Basra Doulla, wakati wa Kikao Kazi cha Kitaalam cha Mnyororo wa Uchunguzi wa Kifua Kikuu kilichofanyika mkoani Morogoro.

Dkt. Doulla amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika rasilimali watu, vifaa vya kisasa na mifumo ya kidijitali ili kuhakikisha huduma za uchunguzi wa kifua kikuu zinapatikana kwa ubora unaohitajika katika maeneo mbalimbali nchini.

Ameongeza kuwa maabara teule za kanda zina mchango mkubwa katika kuimarisha uchunguzi wa kifua kikuu kwa kutoa huduma za vipimo vya ubora wa juu pamoja na kufuatilia mwenendo wa ugonjwa huo, hatua inayosaidia kuongeza ugunduzi wa wagonjwa na kuboresha utoaji wa huduma za matibabu.

“Kipaumbele chetu ni kuhakikisha huduma za maabara za kifua kikuu zinakuwa endelevu na zinapatikana kwa ubora unaohitajika. Hii inajumuisha uwekezaji katika rasilimali watu, vifaa vya kisasa na mifumo ya kidijitali inayorahisisha utoaji wa huduma,” amesema Dkt. Doulla.

Aidha, amesema hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ili kuongeza ubora wa huduma za maabara, ikiwemo kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa vipimo, kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba na vitendanishi pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa maabara nchini.

Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Uchunguzi wa Kifua Kikuu kutoka CIHEB Tanzania, Bw. Samwel Mulungu, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mifumo ya uchunguzi wa kifua kikuu kwa kutumia teknolojia za kisasa zinazowezesha utambuzi wa ugonjwa huo kwa haraka na usahihi zaidi.