SERIKALI YAENDELEA KUI MARISHA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA JAMII
Posted on: June 17th, 2025
Na WAF Tanga
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI inaendelea kutekeleza zoezi la usimamizi shirikishi wa utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii katika mikoa 11 nchini ili kuhakikisha kuwa huduma za afya ngazi ya jamii zinatolewa kwa ufanisi, ubora na kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa.
Wakati wa Utekelezaji wa zoezi hili kwa mkoa Pwani na Tanga, Dkt. Norman Jonas Kyala, Mratibu wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Juni 17, 2025 akiwa mkoani Tanga amebainisha kuwa usimamizi shirikishi ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya afua za afya ngazi ya jamii .
“Usimamizi shirikishi unatuwezesha kuunganisha nguvu za wadau wote katika kubaini mafanikio na changamoto, na kupanga kwa pamoja hatua za kuboresha huduma," amesema Dkt.Kyala.
Amesema Mpango wa Huduma Jumuishi za Afya Ngazi ya Jamii una lengo mahsusi la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zenye kuzingatia mahitaji yao, nyumba kwa nyumba bila kuacha mtu.
Ameongeza kuwa zoezi hilo limehusisha viongozi na wataalam wa afya kutoka ngazi ya kitaifa, mikoa na halmashauri, ambapo timu za wasimamizi zimetoa mrejesho wa moja kwa moja kwa viongozi wa maeneo yaliyotembelewa.
Vilevile, amesema usimamizi shirikishi unasaidia kuimarisha uratibu wa sekta mbalimbali katika utoaji wa huduma za afya ngazi ya jamii na kuhakikisha mpango unatekelezwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa.
Dkt. Kyala amesisitiza kuwa Mpango Jumuishi wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii unatekelezwa kwa kuzingatia dira ya taifa ya kuwa na huduma za afya zinazoratibiwa na kuunganishwa vyema, ili kufikia lengo la afya kwa wote na kuchangia katika kufikia malengo ya UHC (Universal Health Coverage).