Ministry of Health

SERIKALI YA RAIS SAMIA KUIJENGA MUHIMBILI YA KISASA

Posted on: May 11th, 2026

Na Zakayo Mosha WAF-Dodoma

Waziri wa Afya Mhe.Mohamed Mchengerwa ameliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Serikali ya awamu ya Sita Chini ya uongozi shupavu wa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuijenga Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Hayo ameyasema leo Mei 11,2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwakilisha makadirio ya mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya fungu 52 kwa mwaka wa fedha 2026/27

"mradi wa Muhimbili mpya si mradi wa afya pekee, bali ni uwekezaji wa kimkakati katika uchumi wa kisasa,mradi huu utapunguza rufaa za nje, utaongeza tiba utalii, utavutia wawekezaji, mashirika ya Kimataifa na vipaji adimu, na utaifanya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za afya, biashara na uwekezaji wa kikanda" amesema Mchengerwa

Mheshimiwa Mchengerwa amesema kuwa, mwelekeo wa Sekta ya Afya haujajengwa juu ya takwimu peke yake, bali juu ya wajibu wa kulinda utu wa mwananchi.Amesisitiza kuwa Serikali inapoongeza ujenzi wa hospitali inasogeza haki; tunapozalisha dawa nchini, tunajenga uhuru wa afya; tunapounganisha mifumo ya TEHAMA, tunaharakisha maamuzi ya kuokoa maisha, ubora pamoja na kuthibitisha kuwa kila Mtanzania anastahili kuhudumiwa kwa heshima.

"Hii ndiyo falsafa ya maendeleo ya watu ambayo Mwalimu Nyerere aliisimamia, na ndiyo roho ya utu ambayo Mandela aliikumbusha dunia" amesema na kuongeza Waziri Mchengerwa

Ameliambia Bunge kuwa,Serikali imefanya tathmini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili na kubaini changamoto za uchakavu wa miundombinu, kutawanyika kwa majengo, gharama kubwa za uendeshaji na mazingira yasiyoruhusu maboresho ya huduma za ubobezi na teknolojia ya kisasa.amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya Sita imepanga kujenga Muhimbili mpya ndani ya miaka mitano kwa gharama ya Shilingi trilioni 1.2, ambapo Shilingi bilioni 908.6 ni mkopo wenye masharti nafuu na Shilingi bilioni 292 ni mchango wa Serikali kupitia maandalizi ya eneo, misamaha ya kodi, ushuru na tozo.

Mheshimiwa Mchengerwa amesema kuwa kukamilika Kwa mradi huu mkubwa wa Kimkakati kutaifanya Tanzania kuwa na Hospitali kubwa kwa gharama nafuu, chini kwa wastani wa asilimia 42.