SERIKALI, SEKTA BINAFSI KUENDELEZA MAJADILIANO KUELEKEA UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Posted on: March 10th, 2025
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi imeishauri Serikali kupitia Wizara ya Afya iendelee kukutana na wadau wa Sekta Binafsi ikiwemo wamiliki wa hospitali ili kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kuendelea kuboresha Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya sura ya 395 iliyotungwa Mwaka 1999 katika kuelekea utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi Mhe. Cecil Mwambe ametoa mapendekezo hayo leo Machi 8, 2025 wakati wa kuhitimisha kikao cha kamati hiyo pamoja na Serikali kupitia Wizara ya Afya kilichofanyika katika kumbi za Bunge Jijini Dodoma.
"Sisi kama Kamati tunaishauri Serikali kupitia Wizara ya Afya, iendelee kukutana na wadau wake wakiwemo wamiliki wa hospitali na taasisi binafsi ili muweze kujadiliana namna bora ya kuendelea kuboresha Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ya mwaka 1999 kwa manufaa ya wananchi," amesema Mhe. Mwambe
Kwa upande wake, Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameihakikishia kamati hiyo kuwa Serikali pamoja na Sekta Binafsi sio washindani bali ni washirika katika kuendelea kuboresha Sekta ya Afya na hasa baada ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta hiyo ikiwemo kujenga vituo vya kutolea huduma za afya elfu 10,044 nchi nzima kuelekea utekelezaji wa malengo ya kidunia ya utoaji wa huduma za afya kwa wote.
Pia, Waziri Mhagama amesema Wizara ya Afya inaendelea kupitia tena miongozo itakayowezesha Sekta Binafsi kutoa huduma za afya bila kikwazo na kufanya huduma hizo ziweze kufikika kote nchini.
Nae, Mwanasheria wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bw. Matamusi Fungo kwa niaba ya Mkurugenzi wa NHIF Dkt. Irene Isaka wakati akitoa ufafanuzi kuhusu hoja za kamati amesema Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unayo mikakati mbalimbali ya kuhakikisha unakuwa na uhai na uendelevu ikiwa ni pamoja na kufanya tathimini kila baada ya miaka mitatu (3) kwa mujibu wa sheria.