SERIKALI KUFANYA MSAWAZO WA HUDUMA ZA KIBINGWA HOSPITALI ZA KANDA NA HALMASHAURI
Posted on: May 12th, 2026Naibu Waziri wa Afya, Florence Samizi, amesema Serikali imekuja na mpango wa kufanya msawazo wa huduma za kibingwa katika hospitali za kanda kwa kuongeza huduma hizo kutoka huduma nane hadi 17, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote za kibingwa karibu na maeneo yao.
Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Mei 12, 2026, bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge kuhusu utekelezaji wa huduma za afya nchini.
Dkt. Samizi amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga pia kufikisha huduma za kibingwa katika hospitali za halmashauri kwa kuhakikisha kila hospitali ya halmashauri inakuwa na angalau huduma tano za kibingwa ili wananchi waweze kupata huduma hizo kuanzia ngazi ya halmashauri.
“Huduma za kibingwa zimekuwa zikipatikana kwa viwango tofauti; mfano Hospitali ya Lindi bado ina huduma tatu za kibingwa, Tabora sita na Sumbawanga tano. Hivyo, tutafanya msawazo ili huduma hizo zifike kila mahali. Tumeendelea kujipanga kuhakikisha tunatimiza maono ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kufikisha huduma za kibingwa kwa Watanzania. Mheshimiwa Rais amesema wananchi wasizifuate huduma bali huduma ziwafuate wananchi,” amesema Dkt. Samizi.
Aidha, ameeleza kuwa utoaji wa huduma za kibingwa unahitaji uwepo wa rasilimali watu wenye weledi, wataalamu wabobezi pamoja na miundombinu rafiki, hivyo Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya hospitali kuanzia ngazi ya taifa hadi mikoa.
Akitolea mifano ya uwekezaji huo Dkt. Samizi, amesema Mkoa wa Katavi umetengewa shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mama na watoto wachanga, Mkoa wa Rukwa umetengewa shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya kukamilisha jengo la damu salama pamoja na kuanzisha ujenzi wa hospitali mpya na shilingi milioni 542 kwa ajili ya kuanza huduma za uchujaji damu na ukarabati wa wodi hiyo.
Kwa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Samizi amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 4.7 kwa ajili ya jengo la watoto wachanga na shilingi bilioni saba kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma za upandikizaji figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.