Ministry of Health

SERIKALI KUENDELEA KUKARABATI HOSPITALI KONGWE NCHINI

Posted on: May 12th, 2026

Na Mvuda Jaffer,WAF:Dodoma

Serikali imejipanga kuendelea kukarabati hospitali kongwe nchini ili ziweze kuendelea kutoa huduma za afya zinazokwenda sambamba na mahitaji na viwango vya huduma za afya vya wakati wa sasa.

Hayo yamezungumzwa leo Mei 12,2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Florence Samizi kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Tanga, Rashid Shangazi bungeni.

Dkt.Samizi amesema Hospitali ya Bombo ni miongoni mwa hospitali kongwe na chakavu lakini imeendelea kufanya kazi kubwa katika utoaji wa huduma za afya, ambapo kwa sasa inatoa huduma za kibingwa 10 kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo ya jirani.

“Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa wodi za wagonjwa katika Hospitali ya Bombo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha mazingira ya utoaji huduma za afya na kuongeza uwezo wa hospitali hiyo kuhudumia wagonjwa wengi zaidi.”amesema Dkt.Samizi

Pia Dkt.Samizi ameongeza kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la damu salama, hatua inayotarajiwa kuimarisha huduma za uhifadhi na upatikanaji wa damu salama kwa ajili ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

“Maboresho hayo yataongeza ubora wa huduma za afya, kupunguza changamoto za miundombinu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za kisasa karibu na maeneo yao.”amesistiza Dkt. Samizi