Ministry of Health

SERIKALI IWEKEZE ZAIDI KWENYE KINGA KUPUNGUZA MAGONJWA YAKUAMBUKIZA, YASIYOAMBUKIZA

Posted on: May 11th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF - Dodoma

Mbunge wa Buchosa Mhe. Erick Shigongo ameishauri Serikali kuendelea kuwekeza zaidi kwenye huduma za kinga kuliko tiba ili kudhibiti kuenea kwa magonjwa na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika nchini.

Mhe. Shigongo ametoa mapendekezo hayo leo Mei 11, 2026 wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Afya baada ya kuwasilishwa na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa katika Bunge la 13, Mkutano wa Tatu, Kikao cha 26.

"Mhe. Mwenyekiti, kinga ni msingi muhimu wa taifa lenye wananchi wenye afya bora, naiomba Wizara ya Afya iwekeze zaidi kwenye huduma za kinga kuliko kuweza zaidi kwenye tiba," amesema Mhe. Shigongo

Aidha, Mhe. Shigongo amesema uwekezaji katika chanjo, elimu ya afya pamoja na huduma za kinga kwa watoto ni hatua muhimu ya kulinda afya na kupunguza gharama kubwa za matibabu zinazoweza kujitokeza.

"Mhe. Mwenyekiti, taasisi mbalimbali za kimataifa zimekuwa zikisaidia nchi zinazoendelea katika upatikanaji wa chanjo na huduma za afya, hivyo ni muhimu Tanzania kuendelea kushirikiana na wadau hao huku ikiweka mikakati madhubuti ya kuongeza uwezo wa ndani katika sekta ya afya," amesema Mhe. Shigongo