“OPERATION SMILE” YALETA TABASAMU KWA WANYANYAPALIWA
Posted on: May 25th, 2025
Na WAF, Mtwara
Wazazi wa watoto wenye tatizo la mdomo wazi kwa nyakati tofauti tofauti, wameishukuru Kambi ya Uchunguzi, Upasuaji na Matibabu ya tatizo hilo inayoendeshwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Operation Smile Tanzania kwa kusogeza huduma hiyo karibu na kwamba baada ya matibabu hayo imerejesha furaha katika maisha yao.
Wameyasema hayo Mei 24, 2025 kwenye kambi maalum ya upasuaji wa mdomo wazi inayofanyika viwanja vya Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini- Mtwara ambapo wazazi hao wameonesha hali ya kuwa na matumaini ya kurejesha amani na furaha ya familia kwa kupata huduma hiyo inayotolewa bila malipo.
“Nimepitia changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kutengwa na jamii wakiamini kuwa mtoto wangu ni mkosi. Pia baba yake tumeachana kwa kuamini kuwa hawezi kuzaa mtoto kama huyu, lakini mpaka nimefika hapa Mtwara kupata huduma hii nina imani kuwa mtoto wangu atakaa vizuri kwani madaktari wamesema tatizo hili linatibika,” amesema Bi. Swaumu Salimu kutoka Singida.
“Tatizo langu limetokea tangu mwaka 2002 lakini kutokana na kukosa fedha za matibabu nikabaki tu nyumbali, lakini baada ya kupata taarifa ya huduma hizi nikafanyiwa mpango wa kuja kutibiwa. Ninalipongeza Shirika hili kwa kutuletea huduma kama hizi bure na ninawaombea kwa Mungu waendelee kuwa na moyo huu kwani watu wenye changamoto hizi ni wengi na wanaendelea kuzaliwa," amesema Bw. Jamali Saidi Madiva kutoka Mtwara.
Kwa upande wake Meneja Mkazi wa Shirika la Operation Smile Tanzania Dkt. Hamid Mandali amesema kuwa huduma zote zinatolewa bila malipo ikiwa ni pamoja na matibabu, chakula, malazi, usafiri na kuongeza kuwa lengo la kuweka kambi hizi ni kusogeza huduma kwa wananchi na kuwapunguzia gharama za matibabu pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa Tanzania kwani kambi hiyo imehusisha wataalam kutoka nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ethiopia, Malawi, Kenya, Ghana na nchi kutoka Bara la Marekani na Ulaya.
Naye mwakilishi wa Wizara ya Afya Dkt. Alphonce Chandika ameeleza kuwa kambi hiyo inayoendeshwa na madaktari waliobobea kutoka nchi mbalimbali, wastani wa takribani watoto 2000 kwa kila mwaka wanazaliwa na changamoto ya domo wazi. Aidha, Dkt. Chandika amewaasa wataalam wa Tanzania waliopo katika kambi hiyo wawe na moyo wa kujifunza ili wawe na uwezo wa kutoa huduma kama hizo wenyewe.
“Watumishi wetu wa Wizara ya Afya waichukulie kambi hii kama fursa ya kuifunza ili mwisho wa siku watoe huduma hizi wao kama wao pamoja na kujijengea uaminifu wa kuendelea kushirikiana na Shirika hili katika nchi nyingine,” ameongezea Dkt. Chandika.
Kambi ya Uchunguzi, na Mtaibabu ya Mdomo wazi imeanza rasmi Mei 24, 2025 hadi Mei 30, 2025 na imejikita kutoa huduma bila malipo kwa watoto pamoja na watu wazima kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.