Ministry of Health

MWENYEKITI WA KAMATI AIPONGEZA WIZARA YA AFYA KUBORESHA HUDUMA ZA KINGA

Posted on: May 12th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF - Dodoma

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi Mhe. Johanes Lukumay ambaye ni Mbunge wa Arumeru Magharibi ameipongeza Wizara ya Afya kwa kazi kubwa inayofanywa katika kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa nchini.

Mhe. Lukumay ametoa pongezi hizo leo Mei 12, 2026 wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Afya baada ya kuwasilishwa na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa katika Bunge la 13, Mkutano wa Tatu, Kikao cha Ishirini na Saba.

"Serikali imefanya maboresho makubwa katika kudhibiti na kutoa elimu kuhusu magonjwa mbalimbali ikiwemo homa ya ini pamoja na kuimarisha afya ya msingi katika jamii," amesema Mhe. Lukumay

Aidha, Mhe. Lukumay amesema Serikali ya awamu ya Sita imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati hali iliyoongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wengi zaidi nchini na kupata huduma hizo ndani ya kilometa Tano.

"Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaofanywa katika Hospitali ya Mloganzila amabo utaisaidia Tanzania kuimarisha huduma za kibingwa, tafiti za afya pamoja na utalii wa tiba kutokana na uwepo wa mitambo ya kisasa ya matibabu," amesema Mhe. Lukumay

Katika mchango wake, Mhe. Lukumay amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza zaidi katika huduma za kinga akieleza kuwa kinga ni njia muhimu ya kupunguza gharama za matibabu na kulinda afya za wananchi.

Mwisho, aliishukuru Wizara ya Afya kwa juhudi kubwa zinazofanywa katika kuboresha sekta ya afya nchini huku akieleza kuwa wananchi wanaendelea kuona matokeo chanya ya uwekezaji huo kupitia huduma bora zinazotolewa katika hospitali na vituo vya afya.