Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MSD YAANZA KUSAMBAZA VIFAA TIBA VYA HUDUMA ZA AFYA YA UZAZI KATIKA MAJIMBO 214 NCHINI.

Posted on: January 18th, 2024


Bohari ya Dawa (MSD) imeanza kutekeleza agizo la Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu la kusambaza vifaatiba vya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto katika Majimbo yote 214 Tanzania bara.

Mnamo Januari 5, 2024 Waziri Ummy Mwalimu akiwa anapokea vifaatiba hivyo Jijini Dar Es Salaam alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanikisha ununuzi wa Vifaatiba hivyo vilivyogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 14.9 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ya uzazi mama na mtoto nchini na kuiagiza MSD kuanza haraka kazi ya usambazaji wa vifaatiba hivyo.

Akipokea vifaatiba hivyo leo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima,amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombonu ya Sekta ya Afya na kwa sasa imejielekeza katika uboreshaji wa viwango vya utoaji wa huduma za afya nchini.

“Malengo yetu sisi Mkoa baada ya kupokea kwa vifaa tiba hivi ni kwenda kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na hili tumekuwa tukilihimiza nyakati zote” Amesema Mhe. Malima .

Mhe. Malima aemesema licha ya kupokea vifaa tiba hivyo, mkakati wa Mkoa ni kuendelea kutoa elimu kuhusiana na kujikunga na magonjwa mbalimbali na namna ya utumiaji wa vifaa hivyo kwa wagonjwa.

Kwa upande wake Meneja wa MSD, Kanda ya Mashariki yenye Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ,Morogoro na Visiwani Zanzibar, Betia Kaema alisema hayo wakati wa makabidhiano wa vifaa hivyo na mkuu wa mkoa wa Morogoro , Adam Malima kwa ajili ya majimbo 11 ya mkoa huo.

Kaema alisema , Mkoa wa Morogoro umepata vifaa aina tisa vyenye thamani ya Shilingi Milioni 759 na kuanza kusambazwa katika majimbo yote 11 na kila jimbo litapokea vifaa vyenye thamani ya Shilingi Milioni 69.

Kaema alivitaja vifaa vilivyokabidhiwa kwa kila jimbo la mkoa huo ni Drip stand (330), vitanda vya kawaida vya wagonjwa (330), vitanda vya kujifungulia mama wanajawazito (220) na seti (220) za kujifungulia mama wajawazito, shuka (1,320), magodoro (330), Examination table (220), meza ndogo za wagonjwa kuwekea vifaa vyao pale wanapokuwa wamelazwa (165) na Bed side Locker (330).