Ministry of Health

MRADI WA PANDEMIC FUND KUIMARISHA USALAMA WA WAGONJWA HOSPITALINI MIKOA MBALIMBALI NCHINI

Posted on: March 13th, 2026

Na Abduly Iddy, Kigoma

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaendelea kutekeleza mradi wa Pandemic Fund unaolenga kuimarisha usalama wa wagonjwa na watoa huduma za afya katika hospitali na vituo vya afya vinavyotoa Huduma za upasuaji katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwemo Ruvuma, Singida, Kagera na Kigoma.

Akizungumza Machi 11, 2026 mkoani Kigoma, Mratibu wa shughuli za mradi huo kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Radenta Bahegwa, amesema mradi huo unalenga kuimarisha uwezo wa mfumo wa afya nchini katika kuzuia, kugundua na kukabiliana na milipuko ya magonjwa huku ukiweka mkazo katika kulinda usalama wa wagonjwa wanaopata huduma hospitalini ,watoa Huduma, Jamii na mazingira Kwa ujumla

Amesema kupitia mradi huo serikali inaimarisha utekelezaji wa afua za kukinga na kudhibiti maambukizo (IPC), kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa yatokanayo na utoaji wa Huduma za afya pamoja na kuboresha ukusanyaji na matumizi ya takwimu za afya.

Kwa mujibu wa Dkt. Bahegwa, mradi huo pia unatekeleza nguzo nane za WHO (WHO 8 Core Components) za udhibiti wa maambukizi, ambapo moja ya vipengele muhimu ni component namba 4 inayotaka nchi kuwa na mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa yanayotokana na utoaji wa huduma za afya (Healthcare Associated Infection Surveillance).

Kupitia hilo, Kitengo cha Uhakiki wa Ubora wa Huduma za Afya kimeanzisha ufuatiliaji wa maambukizi katika maeneo ya upasuaji (Surgical Site Infection Surveillance) huku taarifa zake zikitumwa kupitia mfumo wa DHIS2 ili kusaidia kupanga maboresho ya huduma.

Ameongeza kuwa tathmini ya utekelezaji wa mfumo huo inaendelea kufanyika katika hospitali za halmashauri na vituo vya afya vyenye wagonjwa wengi, ambapo kwa kuanzia zoezi hilo linafanyika Mkoa wa Kigoma,Kagera, Singida na Ruvuma kuanzia Machi 10 hadi 14, 2026.

Mradi wa Pandemic Fund unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, OWM TAMISEMI WHO na wadau wa maendeleo kwa lengo la kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza usalama wa wagonjwa pamoja na wahudumu wa afya nchini.