Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MOLLY SIMS AONGEZA NGUVU UBORESHAJI WA HUDUMA ZA WATOTO NJITI NCHINI

Posted on: August 16th, 2023

Mwanamitindo na Mwigizaji wa Kimataifa Molly Sims ambaye ni Mke wa Mwenyekiti wa Netflix Films, Scott Stuber, amechangia Dola Elfu 25 ambayo sawa na shilingi Milioni 62 za Kitanzania kwa ajili ya ujenzi wa wodi maalum ya watoto wachanga katika hospitali ya Wilaya ya Kwimba.

Bi. Molly amechangia pesa hizo wakati akifungua kampeni ya ujenzi wa wodi maalum ya watoto wachanga wakiwemo watoto njiti katika hospitali ya Wilaya ya Kwimba, wazo lililoanzishwa na Taasisi ya Kimataifa ya JHPIEGO na Doris Mollel Foundation, na kuhudhuriwa na Mkuu wa Idara ya Mama na Mtoto na Afya ya Uzazi wa Wizara ya Afya, Dkt. Felix Bundala pamoja na viongozi kutoka makao makuu ya JHPIEGO duniani.

Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation, Bi. Doris Mollel na Mkurugenzi Mkazi wa JHPIEGO Tanzania Alice Christensen kwa pamoja wameahidi kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kushawishi Wadau wengine na Serikali kuchangia fedha nyingine za kumalizia jengo hilo.

Itakumbukwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alichangia pesa zake binafsi Tsh. Mil 70 kwa ajili ya kutoa hamasa ya ujenzi pamoja na kununua vifaa vya Watoto njiti katika Hospitali hio ya Wilaya ya Kwimba mwaka jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti Duniani yaliyoandaliwa na Doris Mollel Foundation.