Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MIKOA, WILAYA KUENDELEA KUIMARISHWA ILI KUSIMAMIA WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII

Posted on: June 16th, 2025

Na WAF, Lindi


Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dkt. Kheri Kagya, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi uwezo wa mikoa na halmashauri katika kusimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa kazi za Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) ili kuhakikisha huduma bora na zenye ufanisi zinafika moja kwa moja kwa wananchi.


Dkt. Kagya ameyasema hayo leo Juni 16, 2025, alipokutana na timu ya wataalam kutoka Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais – TAMISEMI waliofika ofisini kwake kwa ajili ya zoezi la Usimamizi Shirikishi wa Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii mkoani humo.


Ameeleza kuwa jitihada za Serikali za kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na usimamizi wa CHW zinatoa fursa kwa timu za mikoa na halmashauri kuhakikisha kuwa huduma zinatolewa kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya na mahitaji halisi ya jamii. “Tunapongeza hatua hizi za kuimarisha ufuatiliaji na tunaamini kuwa kuziwezesha timu za mikoa na halmashauri kutafanikisha usimamizi bora hadi ngazi za vitongoji na mitaa ambako CHW wanatumikia jamii zao,” amesema Dkt. Kagya.


Ameongeza kuwa mkoa wa Lindi kupitia halmashauri zake ikiwemo Lindi Manispaa, Mtama, na Ruangwa, umefanikiwa kutoa mafunzo kwa idadi kubwa ya CHW katika vyuo vya afya vilivyopo mkoani Lindi na Mtwara, hatua inayochochea uboreshaji wa huduma za afya ngazi ya jamii.


Kwa upande wake, kiongozi wa msafara kutoka Wizara ya Afya, Bi. Orsolina Tolage, ameeleza kuwa lengo la zoezi la usimamizi shirikishi ni kuhakikisha mpango unatekelezwa kwa ufanisi na huduma zinazotolewa na CHW zinaboresha afya za wananchi.



 Amebainisha kuwa mafunzo ya awamu ya kwanza kwa CHW mkoani humo yalianza Oktoba 2024 na kukamilika Aprili 2025, na kwamba timu hiyo inakusanya taarifa za kina ili kuwa na kanzi data sahihi ya waliohitimu na wanaoendelea na mafunzo.