Ministry of Health

MCHENGERWA ASISITIZA UTOAJI WA HUDUMA BORA ZA AFYA KWA WANANCHI

Posted on: April 2nd, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Dar es Salaam


Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya,huku utoaji wa huduma hizo  ukizingatia misingi thabiti na maadili.


Mhe. Mchengerwa amesema hayo leo, tarehe 2 Aprili 2026, wakati wa kikao kazi na wadau wa sekta ya afya kilichoambatana na ziara ya kutembelea  Bohari ya Dawa (MSD), jijini Dar es Salaam.


Waziri Mchengerwa amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika na  kusogezwa karibu na wananchi, jambo linalorahisisha upatikanaji wa huduma hizo.


Mchengerwa, ameongeza kuwa, uwekezaji katika miundombinu na rasilimali watu umeendelea kuimarishwa, jambo linalosaidia kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa. Utoaji wa huduma bora zinahitaji wataalamu waliokamilika na vifaa vya kisasa, na serikali inaendelea kuhakikisha haya yanapatikana.


Aidha, Waziri Mchengerwa amesema Serikali imeendelea kusisitiza haki ya kila mwananchi kupata huduma bora kwa wakati unaofaa, jambo linaloongeza imani  wananchi katika Sekta  wa afya hapa nchini.